AUC: Raila apata uungwaji kutoka Zimbabwe
NA CHARLES WASONGA
NDOTO ya kiongozi wa Azimio La Umoja-One Kenya la kutaka kutwaa wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) imepigwa jeki baada ya kupata uungwaji mkono kutoka kwa Zimbabwe.
Kwenye taarifa Jumamosi, Rais William Ruto ambaye yuko ziarani nchini humo, alisema Zimbabwe imekubali kuunga mkono Kenya katika kinyang’anyiro hicho “kutokana na uhusiano wa karibu kati ya nchi hizi mbili kwa miaka mingi”.
“Zimbabwe imekubali kuunga Kenya mkono katika juhudi zake za kutwaa uongozi wa Tume ya Umoja wa Afrika huku Kenya ikiunga mkono juhudi za Zimbabwe za kujiunga na Jumuiya ya Madola,” Dkt Ruto akasema kwenye taarifa.
Rais Ruto alisema kuwa Kenya pia itaunga mkono wito wa Umoja wa Afrika (AU) wa kutaka vikwazo vya kiuchumi vilivyowekewa Zimbabwe na Umoja wa Ulaya (EU) na Amerika viondolewe.
“Naridhika kwamba Kenya na Zimbabwe zitaendelea kusaidia na kuunga mkono juhudi zao katika masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa sambamba na Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063,” akaongeza.
Bw Odinga ambaye alitangaza azma yake ya kuwania wadhifa wa AUC Februari 2024 anakabiliwa na ushindani kutoka kwa aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Somalia Fawzia Yusuf Adam na Waziri wa sasa wa Masuala ya Kigeni waa Djibouti Ali Mahmoud Youssouf.
Kufikia sasa Waziri huyo Mkuu wa zamani amepata uungwaji kutoka Uganda, Rwanda, Ghana, Angola, na Guinea Bissau miongoni mwa nchi nyingine.