Azimio yaapa kuzima Mswada wa Fedha 2024
NA SHABAN MAKOKHA
VIONGOZI wa Azimio la Umoja One Kenya wameonya wabunge wa muungano huo dhidi ya kuunga mkono Mswada wa Fedha 2024 wakisema itakuwa sawa na kusaliti raia.
Wabunge wa muungano huo wa upinzani wameapa kuzima mswada huo wakisema utaumiza Wakenya zaidi kutokana na aina mpya za ushuru.
Wakiongozwa na naibu kiongozi wa ODM Wycliffe Oparanya, George Wajackoya na kiongozi wa chama cha DAP Kenya Eugene Wamalwa viongozi hao walikosoa mswada huo wakisema utakuwa na athari hasi kwa Wakenya ambao tayari wamebebeshwa mzigo mkubwa wa kodi na serikali ya Kenya Kwanza.
Bw Oparanya alisema kwamba watoto wengi hawajaweza kurudi shule kwa sababu watoto wao hawawezi kupata karo hali iliyosababishwa na mzigo wa gharama ya maisha tangu serikali ya Kenya Kwanza iongeze ushuru.
“Wakati utafika ambapo tutasema tawe (hapana) tukatae Wakenya kuendelea kunyanyaswa na utawala wa Kenya Kwanza. Wabunge wetu wa Azimio wanapaswa kusimama kidete na kukataa Mswada unaopendekeza ushuru wa kuumiza Wakenya,” alisema Bw Oparanya.
Alisema watafuatilia kwa makini kuona wabunge wa upinzani watakauunga mswada huo.
Bw Wamalwa alihimiza wabunge wa upinzani kupigania haki za Wakenya wa kawaida na kukataa presha kutoka kwa serikali inayolenga kuongeza ushuru.
“Wakenya wamekuwa wakiteseka tangu mwaka 2023 Rais Ruto alipoanzisha ushuru wa juu. Wanatazama wabunge waweze kukataa Mswada wa Fedha 2024. Lazima muwe jasiri na kuokoa nchi kutoka kwa ushuru katili unaoanzishwa na serikali,” aliwashauri wabunge hao.
Bw Wamalwa alisema Mswada wa Fedha 2024 ni mbaya zaidi ya wa 2023.
Wabunge waliohudhuria mazishi ya Agneta Nerima Wangwe, mama ya mbunge wa Navakholo Emmanuel Wangwe katika shule ya msingi ya Sisokhe waliahidi kuungana kuzima Mswada huo walivyofanya walipopitisha hoja ya kumtimua Waziri wa Kilimo Mithika Linturi kabla ya waziri huo kuokolewa na kamati maalumu iliyochunguza madai dhidi yake.
Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya alisema serikali inapaswa kueleza mafanikio ya Mswada wa Fedha 2023 ambao ulianzisha ushuru wa juu.
“Kabla ya Mswada uliopendekezwa wa Fedha 2024 kuletwa bungeni, tunataka Waziri wa Fedha kuitwa na Bunge aeleze kiasi cha jumla cha pesa zilizokusanywa kutokana na Mswada wa Fedha 2023 na jinsi Wakenya wamefaidika kabla ya kujadili Mswada wa Fedha 2024 ambao ni wa bajeti ya Sh3.9 trilioni,” alisema Bw Salasya.
Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi aliwataka wabunge kujiondolea lawama kwa kushirikiana na maseneta na kuacha kuwa vibaraka wa serikali.
Hata hivyo wabunge wa Kenya Kwanza walitetea mswada huo wakisema unanuiwa kuleta maendeleo nchini. Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Taifa kuhusu bajeti Mary Emase alisema miradi kama barabara nzuri na miundomsingi ya shule inahitaji pesa nyingi na inaweza kutekelezwa serikali ikiwa na pesa za kutosha.