Habari za Kitaifa

Azimio yakunja mkia kuhusu mkutano wake wa ‘kufa kupona’

January 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Na CECIL ODONGO

MUUNGANO wa Azimio la Umoja One Kenya umeahirisha mkutano wake ambao ulitarajiwa kuandaliwa Januari 25, 2024 kuamua hatima yake.

Hatua hiyo inakuja wakati ambapo inadaiwa viongozi wake wametofautiana kisiasa kuhusu uchaguzi mkuu wa 2027.

Azimio ilipanga kuandaa mkutano wake Alhamisi kutathmini masuala yanayohusiana na uaminifu wa wanachama wake, kutatua mzozo kati ya vyama tanzu na pia tofauti ambazo zimezuka kutokana na ripoti ya Kamati ya Bomas.

Suala tata hasa linahusu ni nani anayestahili kupeperusha bendera ya Azimio katika kura za 2027 ambalo limeibua joto ndani ya muungano huo, liliratibiwa kujadiliwa.

Bw Odinga hata hivyo mnamo Jumatatu alipuuza madai kuwa kuna mgawanyiko ndani ya Azimio na akasema wataendelea kupigania haki za Wakenya.

Waziri huyo mkuu wa zamani alisema madai kuwa kuna mzozo baina ya vinara wa Azimio hayana msingi.

Hii ni licha ya kuwa baadhi yao wametofautiana vikali hadharani hasa kuhusu Ripoti ya Maridhiano (NADCO).

“Muungano huu ni thabiti na uongozi wake uko makini kuwatetea raia wa kawaida. Tofauti za kimawazo kati ya vinara hazimaanishi kuwa kuna mgawanyiko,” akasema Bw Odinga akiongoza hafla ya kusajiliwa kwa wanachama wa ODM katika Kaunti ya Lamu.

Jumatano, Baraza Kuu la Azimio (NCEC) kupitia mwenyekiti wake Wycliffe Oparanya, lilisema kuwa limeahirisha mkutano uliopangwa kufanyika Alhamisi. ODM kwa sasa inaendelea kuwasajili wanachama wake ili kuongeza idadi yao katika kaunti za Pwani.

“Tumeahirisha mkutano uliostahili kuandaliwa kwa sababu ya mchakato wa kuwasajili wanachama tunaoendeleza kwa sasa. Ratiba ya hafla hizi mbili imegongana na tutatangaza tarehe mpya ya mkutano,” akasema Bw Oparanya.

Gavana huyo zamani ambaye pia ni naibu kiongozi wa ODM, hata hivyo, alisema wako tayari kwa mazungumzo ambayo yatasababisha kusuluhishwa kwa baadhi ya masuala tata ndani ya Azimio.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Chama cha National Liberal Party Ishmael Oyoo alilalamika kuwa Bw Oparanya na ODM waliamua kuahirisha mkutano huo bila vyama tanzu kuhusishwa.

“Huu ni udikteta ambao unaendelezwa na ODM ndani ya Azimio. Ni kama ODM ndiyo Azimio na Azimio ni ODM. Kwa nini ODM inasisitiza kuwa inaahirisha mkutano huo muhimu bila kuhusisha vyama tanzu?”

“Inasikitisha kuwa walichukua hatua hiyo eti kwa sababu tu wanaendeleza usajili wa wanachama wao,” akasema Bw Oyoo. Katibu huyo alisema mkutano wa leo pia ulistahili kutumika kujaza nafasi za baadhi ya wanasiasa ambao walihama na kuelekea Kenya Kwanza kama vile Sabina Chege na Adan Keynan wa Jubilee.

“ODM imekuwa ikionyesha mapuuza kwa vyama vidogo vidogo licha ya kuwa ni wao ndio walikuja kwetu na kutuomba tuwaunge mkono 2022. Hatutaendelea kuvumilia udikteta wa ODM,” akaongeza.

Mkutano huo ulipaswa kuandaliwa katika makao makuu ya Azimio, Lang’ata South, Nairobi kuanzia saa sita unusu mchana, kwa mujibu wa barua ambayo Bw Oparanya aliandikia vyama tanzu.