Habari za Kitaifa

Azimio yamkaba koo Wetang’ula

Na JOSEPH WANGUI March 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KWA mara nyingine, muungano wa Azimio la Umoja One Kenya umepata ushindi katika mzozo kuhusu mrengo ulio wa wengi baada ya mahakama ya rufaa kukataa kusimamisha uamuzi kwamba una idadi kubwa ya wabunge katika Bunge la Kitaifa.

Uamuzi huo ni pigo kwa Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wa, baada ya majaji kukataa ombi lao la kusimamisha utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama Kuu uliobatilisha tangazo la spika kuwa muungano wa Kenya Kwanza una wabunge wengi.

Mahakama hiyo ilikataa hoja kwamba Bw Wetang’ula alikuwa katika hatari ya kupata ‘fedheha kubwa’ na kwamba anaweza ‘kupata msongo wa mawazo na kudharauliwa’ iwapo uamuzi huo utatekelezwa, kwani tayari anakabiliwa na kesi ya kudharau mahakama kwa madai kwamba alikaidi uamuzi huo.

Ili kuonyesha ukubwa wa mzozo huu, viongozi wa Azimio Junet Mohammed (Kiongozi wa Wachache) na Robert Mbui (Naibu Kiongozi wa Wachache) walijiunga na wanaharakati mahakamani wakitaka Bw Wetang’ula aadhibiwe kwa madai ya dharau ya mahakama.

Bw Junet na Bw Mbui walipinga ombi la kusimamisha uamuzi huo wakisema kuwa ni ‘batili kisheria’ na kwamba Bw Wetang’ula alikaidi Mahakama Kuu kwa kutangaza tena Kenya Kwanza kuwa muungano ulio na wabunge wengi mnamo Februari 12, 2025.

“Bunge la Kitaifa na Spika wake hawakufika mahakamani kwa nia njema, kwani Spika alikaidi Mahakama Kuu alipotoa uamuzi wake Februari 12, 2025 akitangaza Kenya Kwanza kuwa muungano wa wengi katika Bunge la Kitaifa,” walisema Bw Junet na Bw Mbui.

Mahakama ya Rufaa iliombwa kupitia maombi matano kusimamisha utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa Februari 7, 2025, ambao ulifuta tamko la Bw Wetang’ula la Oktoba 2022 kwamba Kenya Kwanza ilikuwa una idadi kubwa ya Wabunge.

Katika uamuzi huo, Mahakama Kuu ilitangaza kuwa uamuzi wa Spika wa Bunge uliotangazwa Oktoba 6, 2022 kuhusu muungano ulio na wabunge wengi na ulio na wachache katika Bunge la Kitaifa ulikiuka Kifungu cha 108 cha Katiba na kwa hivyo, haukuwa halali.

Aidha, Mahakama Kuu ilibaini kuwa Spika wa Bunge hawezi kuwa kiongozi wa chama cha kisiasa akihudumu.

Bw Wetang’ula ni kiongozi wa chama cha Ford Kenya.

Maamuzi haya yalitokana na kesi iliyowasilishwa na wanaharakati 12 wakiongozwa na wakili Kibe Mungai, wakidai kuwa kwa mujibu wa matokeo rasmi ya Uchaguzi Mkuu yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi (IEBC), Azimio ilikuwa na wabunge 171 dhidi ya 165 wa Kenya Kwanza.

Baada ya hukumu hiyo, Bw Wetang’ula, Bunge la Kitaifa, viongozi wa UDA bungeni-Bw Ichung’wa, Owen Baya, Silvanus Osoro, na Naomi Jillo, muungano wa Kenya Kwanza na chama cha Maendeleo Chap Chap walikata rufaa na maombi ya kusimamisha utekelezaji wa uamuzi huo.

Walitaka mahakama itoe agizo la muda kusitisha utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama Kuu hadi rufaa zao zisikilizwe na kuamuliwa.

Hata hivyo, Majaji Daniel Musinga, Mumbi Ngugi, na Francis Tuiyott walikataa ombi hilo wakisema kuwa ingawa rufaa inayosubiri kusikilizwa inaweza kuwa na msingi, walalamishi walishindwa kuthibitisha watakavyoathiriwa iwapo uamuzi uliopo utatekelezwa.

“Kiwango cha kuthibitisha umuhimu wa kutoa agizo la muda katika masuala ya Katiba au ya maslahi ya umma ni cha juu zaidi kuliko katika kesi za kibinafsi. Hatujaridhika kuwa kiwango hicho kimetimizwa katika maombi haya,” walisema majaji hao.

Kuhusu hoja ya Bw Wetang’ula kwamba anakabiliwa na hatari ya kuitwa mahakamani kwa kesi ya kudharau korti, majaji walisema hilo haliwezi kuwa sababu ya kusimamisha utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama Kuu.

“Uwezekano wa mtu kuitwa mahakamani kujibu shtaka la dharau hauwezi kuwa sababu ya kusitisha utekelezaji wa uamuzi wa mahakama,” walisema majaji.

Pia, walishuku kwa nini Bw Wetang’ula alikuwa akiomba mahakama impe agizo la muda dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu huku wakati huohuo akidai kuwa tayari ametii uamuzi huo.