Habari za Kitaifa

Baada ya baridi kali, Wakenya waonywa kuhusu kiangazi kirefu

Na  NDUBI MOTURI September 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAKAZI wa maeneo mengi nchini wakiwemo wa eneo la Ziwa Victoria, Bonde la Ufa Kusini na Kati, nyanda za Juu Mashariki mwa Bonde la Ufa na Nairobi, wameshauriwa kujiandaa kwa mvua chache na vipindi virefu vya ukame kati ya Oktoba–Novemba–Desemba 2025, kwa mujibu wa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Kenya.

Kulingana na Idara hiyo, mvua haitakuwa ya kutosha nchini, huku maeneo mengi yakitarajiwa kupata mvua ya chini ya wastani. Maeneo kama Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Uasin Gishu, Pokot Magharibi, Nandi na Baringo Magharibi yanatarajiwa kupata mvua ya wastani hadi juu kiasi.

Hata hivyo, sehemu kama Turkana, Samburu Mashariki, Marsabit na Kusini Mashariki zinatarajiwa kuwa na ukavu.Maeneo ya karibu na Ziwa Victoria kama Siaya, Kisumu na Migori yatapokea mvua ya wastani hadi chini ya wastani, huku baadhi ya sehemu za Busia zikitarajiwa kuwa kame.

Nairobi na maeneo ya milimani Mashariki mwa Bonde la Ufa kama Nyeri, Murang’a na Kiambu pia yatapata mvua chache.Idara inatahadharisha kuwa hali hii itazidisha changamoto za kiangazi, hasa katika maeneo ambayo tayari yanakabiliwa na ukame. Wakazi wanashauriwa kuchukua hatua mapema ili kukabiliana na hali hiyo