Habari za Kitaifa

Baadhi ya shule zahiari kukaa na wanafunzi waliowasili ili kufanya marudio ya masomo

April 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA TITUS OMINDE

BAADHI ya shule ambazo wanafunzi walikuwa tayari wameshawasili kwa Muhula wa Pili zimehiari kukaa nao na kushiriki marudio hadi wengine warejee kuendelea na masomo.

Katika Shule ya Upili ya Paul Boit Boys, Eldoret, wanafunzi wa Kidato cha Nne tayari walikuwa wameripoti

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Shem Busolo alisema wanafunzi wote wa Kidato cha Nne wapo shuleni na hatawarudishwa nyumbani.

“Tutawahifadhi wanafunzi wetu shuleni ili kuendelea na marudio ya masomo huku tukisubiri wengine wafungue kwa mujibu wa tangazo la Wizara ya Elimu,” alisema Bw Busolo.

Wakati huo huo, wanafunzi ambao wazazi wao hawakupokea tangazo la Wizara ya Elimu kuhusu kuahirishwa kwa shule kufunguliwa kutokana na janga la mafuriko nchini walipigwa na butwaa katika vituo vya kuabiri magari mjini Eldoret.

Ilibidi baadhi ya wahudumu wa magari kuingilia kati ili kuwasaidia kurejea nyumbani kufuatia tangazo hilo.

Baadhi ya wanafunzi ambao Taifa Leo ilizungumza nao walikuwa wasichana wa Singore, St Joseph Boys Kitale, St Annessens Burnt Forest, Bunyore Girls kutoka Kaunti ya Vihiga miongoni mwa shule nyingine.

“Serikali lazima ikomeshe siasa kwa kila kitu, unafanyaje tangazo zito hivyo usiku wa manane ukitarajia wazazi wote watapata habari usiku wa manane? Mbona serikali kutoa tangazo muhimu kama hilo usiku wa manane?” alishangaa Joseph Kiprono, mzazi ambaye tayari alikuwa amemwachilia mwanawe kwenda shuleni.

Bw Kiprono alishutumu Wizara ya Elimu kwa kuchukulia masuala muhimu kimzaha.

Alisema ni jambo la kusikitisha kwa serikali kusubiri hadi usiku wa manane ili kutoa tangazo hilo zito licha ya viongozi wa upinzani wakiongozwa na Eugene Wamalwa kushauri serikali kuahirisha ufunguzi wa shule.

Mzazi mwingine alisema kuwa tangazo hilo liliwashtua wazazi wengi ambao tayari walikuwa wameachilia watoto kusafiri shuleni kabla ya tangazo husika.