Habari za Kitaifa

Baadhi ya wamiliki wa ardhi ya Kibiko wataka utoaji hati miliki usitishwe

Na  STANLEY NGOTHO November 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Baadhi ya wakazi wanaodai ardhi ya kijamii ya Kibiko mjini Ngong, Kaunti ya Kajiado Magharibi, imewasilisha ombi kwa serikali kusitisha mchakato unaoendelea wa utoaji wa hati miliki za ardhi hiyo ya pamoja, wakilalamika kwamba kuna udanganyifu na migogoro ambayo haijatatuliwa.

Mamia ya wanajamii wanaoishi katika ardhi  hiyo ambao wanamiliki ardhi ya ukubwa wa ekari 2,862 ya thamani ya Sh 100 bilioni, wamelalamika kuwa mchakato huu umejaa udanganyifu na umeleta mvutano na ukosefu wa usalama katika eneo hilo.

Katika mkutano wa dharura uliofanyika Jumatatu, baadhi ya wanachama waliochukizwa walisema mchakato wa utoaji wa hati unaofanywa na Wizara ya Ardhi ni kinyume na mapenzi ya wanachama halali, hasa ikizingatiwa  kuna kesi  inayoendelea Mahakama ya Rufaa kuhusu migogoro ya usimamizi wa ardhi hiyo. Uamuzi wa kesi hiyo unatarajiwa kutolewa Januari 30, 2026.

Kundi linalotoa hati miliki linaongozwa na Moses Monik, jambo ambalo linapingwa na kundi la Bw Moses Parantai. Pande zote mbili zinadhibiti wanachama zaidi ya 16,000.

Mweka Hazina wa Keekonyokie Community Trust, Lawrence Ole Mbelati, akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa muda mrefu Moses Parantai, aliomba serikali kusitisha mchakato huu wa utoaji wa hati pamoja na kuchukua hatua nyingine kali ili kuzuia kuenea kwa ghasia.

“Tunaomba serikali isitishe mara moja utoaji wa hati zote zisizo halali hadi pale uchunguzi utakapoisha. Pia tunadai kufutwa kwa uongozi haramu na kuandaliwa kwa mchakato wa uwazi unaoongozwa na jamii kuchagua wadhamini halali,” linasema  sehemu ya ombi hilo.

Wanajamii hao pia wanataka ulinzi dhidi ya unyanyasaji unaodaiwa kufanywa na polisi na maajenti wa wanasiasa.

Wanachama wa Keekonyokie Community Trust wakiwa katika mkutano wa dharura, Novemba 3, 2025. Picha|Stanley Ngotho

Kulingana na wanajamii wanaoishi katika ardhi iliyo kando ya Kaunti ya Kiambu, mvutano unaoendelea kati ya wamiliki halali wa ardhi na watu wanaodaiwa kuiba ardhi umegeuka kuwa tishio la usalama katika eneo ambalo sasa limekumbwa na vurugu.

Kesi nyingi za moto, mashambulizi na vitisho zimeripotiwa katika kituo cha polisi cha Ngong.

“Wanawake na watoto ndio wanaosumbuka zaidi kutokana na mvutano huu, huku makundi mawili yakivutana. Serikali imetuacha peke yetu,” alisema Bi Flora Nkalo, mwanachama.

Wanajamii sasa wanaomba Rais William Ruto kuingilia kati ili kutafuta suluhisho kwa mgogoro huu wa ardhi unaoweza kuharibu jamii.

“Tumepoteza imani kwa taasisi na maafisa mbalimbali wa serikali ambao wamekuwa wakiongeza tatizo kwa maslahi yao binafsi. Tumeweka matumaini yetu kwa Rais William Ruto,” alisema Lepeyion Pariken, mwanachama.

Ardhi  hii ya jamii imekuwa ikikabiliwa na migogoro ya uongozi kwa miaka kadhaa, jambo ambalo limechelewesha kugawanywa kwake kwa wanajamii binafsi wapate hati miliki zao