Baba alifariki mikononi mwangu, afichua Winne Odinga
Binti wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Amolo Odinga, Bi Winnie Odinga, amefichua kwa uchungu kwamba baba yake alifariki mikononi mwake walipokuwa wakitembea pamoja nchini India.
Akizungumza kwa hisia kali wakati wa ibada ya wafu ya baba yake katika Uwanja wa Nyayo, Winnie alikanusha uvumi uliokuwa ukienezwa mitandaoni kwamba Raila alifariki akiwa hali mahututi kitandani. Badala yake, alisema kuwa Raila alikuwa akifanya mazoezi kila siku na alikuwa na nguvu hadi dakika ya mwisho.
“Nilikuwa naye India alipotoa pumzi ya mwisho. Alifariki mikononi mwangu, lakini hakufa kama watu wanavyosema kwenye mitandao,” alisema Winnie mbele ya viongozi na maelfu ya waombolezaji waliokusanyika.
Alieleza kuwa Raila alikuwa akiamka na kutembea, akiongeza hatua kila siku. “Alikuwa akifanya mizunguko – siku ya kwanza mmoja, siku iliyofuata miwili, na siku hiyo alijitahidi akafanya mizunguko mitano. Alifariki akiwa na nguvu, heshima na fahari.”
Winnie alimtaja Raila kama baba mwema na kusema alikuwa msichana mwenye bahati zaidi duniani kwa kuwa mwana wa mtu wa aina hiyo. Aliongeza kuwa ndugu zake, marehemu Fidel, Rosemary na Junior, walikuwa na bahati hiyo hiyo ya kipekee.
Tangu kifo cha Raila kitangazwe rasmi, Winnie amekuwa akisifiwa kwa ujasiri wake mkubwa, akiwa mtoto wa pekee aliyekuwa na baba yake wakati wa kifo chake.
Alipowasili nchini Alhamisi asubuhi, Winnie alishuka akiwa amebeba kofia nyeupe aliyopenda kuvaa baba yake kwa heshima.
Winnie alimkabidhi mama yao, Bi Ida Odinga, kofia hiyo katika tukio lililowagusa sana Wakenya wengi.
Rosemary, mtoto wa pili lakini mkubwa zaidi baada ya kifo cha kifua mimba Fidel Odinga, ndiye aliyeanza kutoa heshima zake kwa baba yao katika uwanja wa Nyayo.
“Baba hakuwa mshauri wangu tu, bali pia rafiki yangu. Nakumbuka nilipopokea habari za kifo chake. Nilikuwa nimekaa mezani nikimalizia kiamsha kinywa changu, ndipo ndugu yangu mdogo alinipigia na kuniuliza nilipokuwa. Nilipomwambia niko mezani, aliniambia niketi,” alisema Rosemary kwa sauti ya huzuni.
Raila Junior, mvulana wa pekee aliyesalia baada ya kifo cha Fidel, alitambua mzigo mkubwa uliomwangukia kama mwanamume wa pekee katika familia hiyo.
“Ninatambua wazi kuwa baada ya kuondoka kwa kaka yangu Fidel, mimi ndiye niliyebaki kama mvulana wa pekee. Baba, nataka kukuhakikishia kuwa nitaitunza familia yetu – Mama, Rosie, Winnie – na hata familia kubwa ya kisiasa uliyokuwa ukiongoza. Asante kwa zawadi ya maisha na kwa kunipa jina lako,” alisema Junior.