Habari za Kitaifa

Baba apinga bintiye kuachiliwa kwa dhamana katika kesi ya mauaji ya Maigo

January 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

BABA yake msichana anayekabiliwa na shtaka la kumuua aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Fedha Nairobi Hospital Eric Maigo, ameomba Mahakama Kuu isimwachilie kwa dhamana kwa vile “atatoroka”.

Bw Zebedeyo Onchari amefichua katika hati ya kiapo aliyowasilisha mahakamani kwamba Anne Adhiambo Ouma almaarufu Nut “haaminiki na tabia yake imepotoka.”

“Hii mahakama iko na haki ya kumnyima dhamana Adhiambo aliyekana kumuua Eric Maigo Onchari usiku wa Septemba 15, 2023, kutokana na tabia yake,” asema Bw Onchari katika ushahidi wake kwa mahakama.

Baba huyo amesema kuwa bintiye alitoroka nyumbani kujificha katika makazi ya mpenziwe. Alionekana katika maeneo ya Bombolulu na Olympics Kibra, Nairobi.

Alitiwa nguvuni Septemba 26, 2023, eneo la Olympics na polisi baada ya picha yake kusambazwa katika vyombo vya habari na pia mitandao ya kijamii.

“Nakubaliana na upande wa mashtaka kwamba mshtakiwa hastahili kuachiliwa kwa dhamana kwa vile hana makao maalum,” Bw Onchari asema katika afidaviti aliyowasilisha kwa mahakama.

Pia mahakama imeelezwa na Bw Onchari kwamba mshtakiwa amekataa kuchukua kitambulisho licha ya kutimiza umri wa kuchukua kitambulisho.

Bw Onchari amesema endapo mshtakiwa ataachiliwa kwa dhamana atawatisha mashahidi ikitiliwa maanani aliwahi toroka taasisi ya kurekebisha tabia ya Dagoretti Girls Rehabilitation mnamo Machi 9 2022.

Adhiambo alikuwa ameagizwa na mahakama ya Kibera Julai 28 2017 apokee mafunzo na kurekebishwa tabia alipohukumiwa kwa makosa ya wizi.

“Mshtakiwa alikuwa ametoroka kwa makazi ya mama yake eneo la Bombolulu hadi alipokamatwa Septemba 26,2023,” baba yake amefichua.

Amesema polisi waliopekua makazi yao walipata nguo alizokua amevaa Adhiambo siku ile Maigo alipouawa.

Mahakama imeelezwa mshtakiwa atatoroka endapo ataachiliwa kwa dhamana.

Wakili Ndegwa Maina anayemtetea mshtakiwa aliagizwa jana na Jaji Diana Kavedza awasilishe ushahidi kwamba mshtakiwa hatatoroka iwapo ataachiliwa kwa dhamana.

Jaji Kavedza aliamuru wahusika wote katika kesi hiyo wawasilishe ushahidi wao kabla ya mahakama kuamua ikiwa itamwachilia mshtakiwa kwa dhamana au la mnamo Februari 21, 2024.

Upande wa mashtaka umepinga mshtakiwa akipewa dhamana ukidai atawavuruga mashahidi na “hana makao maalum jijini Nairobi.”

Adhiambo aliishangaza mahakama alipokiri alimuua Maigo alipofikishwa kortini mara ya kwanza mbele ya Jaji Kanyi Kimondo.

Mnamo Oktoba 26,2023  Adhiambo alikiri alimuua Bw Maigo aliposomewa shtaka mbele ya Jaji Kimondo lakini jaji huyo akaamuru mshtakiwa apewe muda wa kutafakari maungamo yake.

Baadaye alibadilisha nia na kukana mashtaka.

Kesi hiyo inasikilizwa na Mahakama Kuu, Kibra.

Kesi hiyo iliendelea kwa njia ya mtandao.

Kiongozi wa mashtaka Allan Mulama alipinga ombi la mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana akisema atatoroka.

Bw Mulama alisema tabia ya mshtakiwa kuhepa na kujificha kwa zaidi ya mwezi baada ya mauaji hayo ni ishara kwamba mshtakiwa atachana mbuga na kutokomea kabisa.

Pia mahakama ilifahamishwa mshtakiwa hana mahala maalum pa kuishi jijini Nairobi.

Jaji alifahamishwa polisi walimkuta mshtakiwa amejificha katika mtaa wa mabada wa Kibra.

“Mshtakiwa atatoroka akiachiliwa na isitoshe, polisi hawajui mahala wanaweza kumpata,” Bw Mulama alimweleza Jaji Kavedza.

Pia alisema adhabu kali itakayotolewa dhidi ya mshtakiwa akipatikana na hatia ni “kivutio chake kutoroka akiachiliwa kwa dhamana.”

Mshtakiwa alitiwa nguvuni Septemba 26, 2023, katika eneo la Olympic Kibra baada ya Maigo kuuawa kwa kudungwa kisu mara 25.

Mshtakiwa anazuiliwa katika gereza la wanawake la Lang’ata, Nairobi.