Baba wa Afrika? Raila kukabana koo na wapinzani wake Ijumaa kwenye mjadala wa AUC
MBIVU na mbichi itajitokeza kwenye kinyang’anyiro cha uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) Ijumaa, Desemba 13, 2024 Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga atakapogaragazana na wapizani wake wawili kwenye mdahalo utakaopeperushwa kwenye runinga kote Afrika.
Bw Odinga atashiriki jukwaa moja na wapinzani hao, Mohmoud Ali Youssouf wa Djibouti na Richard Randriamandrato wa Madagascar, kila mmoja akifafanua maono yake mbele ya hadhira itakayojumuisha wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Afrika na Kamati ya Wawakilishi wa Kudumu (PRC), jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Kwenye ukumbi ambako mdahalo huo, almaarufu “Mjadala Afrika” utaendeshwa pia watakiwemo Makamishna wa AU, wanahabari na wageni wengine maalum.
Kwenye taarifa, Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) inasema mdahalo huo unatoa jukwaa kwa wawaniaji kuelezea ndoto zao katika kutimiza lengo la AU la kusuka bara la Afrika lenye umoja, amani na ufanisi.
“Mjadala huo utapeperushwa mubashara kuanzia saa moja jioni, saa za Afrika Mashariki kote Afrika na nje. Aidha, utapeperushwa kupitia tovuti ya AU na mashirika ya habari ya mataifa wanachama,” taarifa hiyo ikaeleza.
Aidha, ikasema, mjadala huo utapitishwa kwa lugha sita rasmi za AU ambazo ni; Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu, Kireno, Kihispania na Kiswahili.
Mjadala huo utakita katika masuala ya kisera huku kila mgombeaji akielezea jinsi analenga kufanikisha kufikiwa kwa Ndoto na Malengo ya Agenda ya AU ya 2063 na utekelezaji wa miradi na mipango yenye umuhimu kwa Afrika na Watu wake.
Wakati wa mjadala huo, unaoashiria kilele cha kampeni za uenyekiti wa AU, wagombeaji pia wataonya uelewa wao wa changamoto zinazoisibu Afrika huku akipendekeza namna ya kuzitatua.
Miongoni mwa changomoto hizo ni; mapigano, misukosuko ya kisiasa, mapinduzi ya uongozi haswa magharibi mwa Afrika, ukame, baa la njaa, makali ya babadiliko ya tabianchi, miongoni mwa zingine.
Tume ya AUC imetoa wito kwa umma kutuma masuala yao kwa wagombeaji hao kupitia sehemu ya kutolea maoni katika mtandao wa kijamii wa X, wakitaja majina yao na nchi waliko wanapofuatilia mjadala huo.
Mdahalo huo unajiri baada ya Bw Odinga kukamilisha ziara yake katika mataifa ya Kaskazini mwa Afrika kusaka kura kutoka marais na viongozi wa nchi hizo.
Majuma mawili yaliyopita Waziri huyo Mkuu wa zamani alibisha hodi katika mataifa mbalimbali ya Afrika Magharibi.
Mnamo Agosti mwaka huu, Bw Odinga alipata uungwaji mkono kutoka kwa marais sita ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Wadadisi wanasema Bw Youssouf, ambaye ni Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Djibouti ndiye mpinzani mkuu wa Bw Odinga, kwa misingi kuwa anaungwa mkono na mataifa mengi yanayozungumza Kiarabu na Kifaransa.