Baraza la wazee laanza msako wa siku 100 wa kubaini wale ambao hawajatahiriwa
BARAZA la Wazee la Jamii za Mlima Kenya, Kiama Kia Ma, limeanzisha msako wa siku 100 wa kubaini wazee wa jamii za Gema ambao hawajatahiriwa, hatua inayozua mjadala kuhusu faragha na mila.
Mlezi wa kitaifa wa baraza hilo, Kung’u Muigai, alisema zoezi hilo linawalenga wazee wote 3,674 waliosajiliwa kuendesha shughuli za kitamaduni.
Alisema kila mzee atalazimika kuthibitisha kuwa ametahiriwa, huku zoezi hilo likifanywa kwa hiari na kwa faragha katika madhabahu ya kitamaduni.
Muigai alisema suala hilo lilijadiliwa katika mkutano wa wazee 63 uliofanyika Kaunti ya Kiambu Septemba 28, baada ya kile alichokitaja kuwa mgogoro wa kitamaduni uliosababishwa na migawanyiko na tamaa.
Alisema tangu 2010, visa 340 vya wazee ambao hawajatahiriwa vimeripotiwa, huku 146 vikigunduliwa baada ya vifo vyao.
Wazee watakaokataa kushiriki zoezi hilo wataondolewa kwenye sajili ya wanaoruhusiwa kutekeleza majukumu ya kitamaduni.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Kikuyu, Wachira Kiago, alisema tohara ni sehemu muhimu ya utambulisho wa jamii, akisisitiza kuwa baraza linapendelea mazungumzo badala ya vurugu.
Muigai alisema baadhi ya wazee wamefichuliwa baada ya kugombana na wake zao, huku wengine wakigunduliwa walipolazwa hospitalini.
Alifichua kuwa mzee mwenye umri wa miaka 72 kutoka Meru alishawishiwa kutahiriwa miaka miwili iliyopita. Wengine watatu wenye umri wa miaka 65, 68 na 74 kutoka Kiambu wanapona baada ya kufanyiwa tohara mwezi huu. Mwingine mwenye miaka 59 kutoka Murang’a anadaiwa kutoroka baada ya kuripotiwa na mkewe.
Kwa mujibu wa Muigai, tangu 2010, visa 340 vya wazee ambao hawajatahiriwa vimeripotiwa, huku 146 vikigunduliwa baada ya vifo vyao.
Alisema wazee watakaokataa kushiriki zoezi hilo wataondolewa kwenye sajili ya wanaoruhusiwa kutekeleza majukumu ya kitamaduni.
Bw Joseph Kaguthi, mratibu wa baraza linalowakutanisha wazee wa Gema na viongozi wa dini, alisema mwanaume ambaye hajatahiriwa haruhusiwi kushiriki katika mikutano ya wazee, kufanya maamuzi ya kitamaduni au kutekeleza baadhi ya mila.
Hata hivyo, mwanahistoria wa tamaduni, John Njue, alisema umuhimu wa kitamaduni wa tohara umepungua kwa miaka mingi, hasa baada ya hospitali na makanisa kuanza kushiriki katika shughuli hiyo.