Jukumu nzito la Gachagua akipanga upinzani kuelekea 2027
KIONGOZI wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, anaonekana kujipa jukumu la kuunganisha viongozi wa upinzani ili kumkabili Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Hata hivyo, haijabainika iwapo viongozi wengine wamekubaliana naye kuongoza juhudi hizo au amejipa jukumu hilo mwenyewe. Mafanikio au makosa yake yanaweza kuamua iwapo atakuwa mgombea muhimu, atafanya mwingine kuingia Ikulu au kumsaidia Ruto kupata muhula wa pili kwa ushindi mkubwa.
Mchambuzi wa siasa Herman Manyora anasema mpango huo una nafasi ya kufanikiwa, ingawa si rahisi.
“Mradi kuna uwezekano hata mdogo wa kufanikiwa, hatuwezi kuupuuza. Siasa ni sanaa ya kufanya yanayowezekana na ndoto zote zina nafasi,” alisema.
Gachagua anaamini eneo la Mlima Kenya ndilo lenye wapiga kura wengi na kwamba bado ana ushawishi mkubwa miongoni mwao. Anadai kuwa nyumbani kwake Wamunyoro, ambako Ruto alikuwa akitembelea mara kwa mara, kulichangia safari ya kisiasa iliyomfanya rais mwaka 2022.
“Naomba ajaribu kukanusha. Alitembelea nyumbani kwangu mara nyingi na mke wangu alimwandalia chakula na kumuombea,” alisema Gachagua.
Mjadala kuhusu mipango yake ulipamba moto baada ya kurejea kutoka Amerika Oktoba 20, baada ya kukaa huko kwa zaidi ya siku 50, na kukutana na kiongozi wa Linda Mwananchi, Edwin Sifuna, nyumbani kwake Wamunyoro.
Washirika wake wanapendekeza kuwa viongozi watatu wenye uwezo mkubwa wa kuvutia wapiga kura ni Gachagua, Sifuna na Kalonzo Musyoka.
Mwenyekiti wa DCP anayehusika na wazee mashuhuri, Maina Kamanda, anasema viongozi hao watatu wana uwezo wa kubadilisha mwelekeo wa siasa na kuvutia idadi kubwa ya wapiga kura.
Hata hivyo, muungano wa upinzani pia una viongozi wengine, wakiwemo Fred Matiang’i, Martha Karua, Eugene Wamalwa, Justin Muturi, Boniface Mwangi, David Maraga, Jimmi Wanjigi na Okoiti Omtatah.
Kwa mujibu wa mkakati unaohusishwa na washirika wa Gachagua, anataka kupunguza kura milioni 7.17 ambazo Ruto alipata mwaka 2022.
Gachagua anaamini kuwa anaweza kuvuta takriban kura milioni 3.5 za Mlima Kenya ambazo zilimsaidia Ruto kushinda. Akiondoa kura hizo, anahesabu kuwa Rais atabaki na takriban kura milioni 3.68.
Anapojumlisha kura hizo 3.5 milioni na kura milioni 6.94 ambazo Raila Odinga alipata mwaka 2022, anafikia jumla ya takriban kura 10.44 milioni akisema hesabu hizo zinaonyesha Ruto anaweza kushindwa.
Lakini Mbunge wa Laikipia Mashariki, Mwangi Kiunjuri, anapinga dhana hiyo. Anasema Gachagua hapaswi kuwania urais wala naibu wa rais.
Kiunjuri anaonya kuwa Gachagua akitengwa na viongozi wengine kwa sababu ya kile anachokitaja kuwa tabia ya kutaka kutawala wengine, anaweza kubaki na chama chake na kura za Mlima Kenya, huku Ruto akipata nafasi ya kushinda tena.
Anasema Ruto anaweza kuvutia takriban kura milioni nne za wafuasi wa Raila, na kuziunganisha na kura milioni tano anazokadiria anaweza kupata, hivyo kufikisha zaidi ya milioni tisa.
Mwanasayansi wa siasa John Okumu pia anaonya kuwa hesabu za upinzani zinaweza kuonekana nzuri hadi pale hatua za Ruto za kuimarisha uungwaji mkono wake zitakapozingatiwa.
Okumu anasema Ruto aliposhirikiana na Raila baada ya kumwondoa Gachagua katika wadhifa wa naibu wa rais, alilenga kuvutia sehemu ya kura za Raila kutoka maeneo nje ya Mlima Kenya. Anasema uteuzi wa Profesa Kithure Kindiki kama naibu wa rais pia ulilenga kumtenga Gachagua kisiasa.
Mbunge wa Homa Bay, Peter Kaluma, anasema Ruto ana nafasi ya kurithi maeneo yaliyokuwa ngome za Raila.
“ Kiongozi wetu aliyeaga dunia alituacha katika serikali jumuishi, na mabadiliko ya utawala ni mjadala wa mwaka 2032,” alisema.
Hata hivyo, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya anapinga mtazamo huo. Anasema baadhi ya viongozi waliokuwa na ushawishi katika maeneo ya Raila hawako tayari kuunga mkono Ruto, akitaja Kalonzo, Wamalwa, Babu Owino, James Orengo na Sifuna.
Mchambuzi Festus Wangwe anasema kwa sasa hesabu za kisiasa zinaonyesha Gachagua, Sifuna na Kalonzo wana nafasi ya kuvutia wapiga kura.
Mkakati wa Wamunyoro unaangazia uwezekano wa tiketi tano za urais na naibu wa rais.
Pendekezo la kwanza ni Kalonzo kuwania urais huku Sifuna akiwa mgombea mwenza, mchanganyiko unaolenga kuunganisha uzoefu na nguvu za vijana.
Pendekezo la pili ni Sifuna kuwania urais huku Kalonzo akiwa naibu wake. Wanaounga mkono mpango huo wanaamini unaweza kuongeza ushiriki wa vijana katika uchaguzi.
Pendekezo la tatu ni Sifuna kuwania urais huku Gachagua akiwa mgombea mwenza. Mchambuzi Malila Munywoki anasema mpango huo unaweza kuvutia kura za Mlima Kenya, lakini ukakumbana na changamoto ya kukubalika kitaifa kutokana na uchovu wa kisiasa kuhusu kubadilishana uongozi kati ya jamii za Wakalenjin na Agikuyu.
Pendekezo la nne ni Gachagua kuwania urais huku Kalonzo akiwa naibu wake. Munywoki anasema mpango huo unaweza kukabili changamoto za kukubalika nje ya ngome zao.
Chaguo la tano ni Kalonzo kuwania urais huku Gachagua akiwa mgombea mwenza.
Wachambuzi wanakubaliana kuwa mafanikio ya upinzani yatategemea iwapo viongozi hao wataafikiana kuhusu mgombea urais mmoja, kugawana majukumu na kuvutia wapiga kura bila kuruhusu tofauti zao kudhoofisha juhudi za kumkabili Ruto mwaka 2027.