Bastola iliyotumiwa kumuua Were imepatikana, Kanja atangaza
BASTOLA iliyotumiwa kumuua Mbunge wa Kasipul, Charles Ong’ondo Were, imepatikana, na kuashiria ufanisi mkubwa katika uchunguzi wa mauaji hayo.
Akizungumza na vyombo vya habari Alhamisi, Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, alisema ripoti ya uchunguzi wa risasi imeonyesha wazi kuwa bastola ya aina ya Sarsilmaz, iliyopatikana kwa mshukiwa mmoja, ndiyo iliyotumika kumuua Were mnamo Aprili 30.
Bastola hiyo ilipatikana kwa washukiwa wawili waliokamatwa wakiwa na silaha mbili – bastola aina za Retay Falcon na Sarsilmaz – pamoja na begi na viatu vilivyofanana na maelezo ya mavazi ya mshukiwa aliyekuwa katika eneo la tukio.
Ripoti ya uchunguzi wa risasi inahusisha moja kwa moja bastola ya Sarsilmaz na risasi zilizomuua Were — IG Kanja
Silaha hiyo pia imehusishwa na matukio mengine matatu ya wizi wa kutumia silaha katika kaunti za Nairobi na Kiambu.
Uchunguzi wa maiti uliofanywa Mei 2 na Mpasuaji Mkuu wa Maiti wa Serikali, Dkt Johansen Oduor, katika mochari ya Lee, ulibaini kuwa Were alipigwa risasi tano upande wa kushoto wa mwili wake.
Risasi mbili ziliondolewa mwilini wakati wa uchunguzi huo, huku risasi ya tatu ikipatikana ndani ya gari la marehemu. Risasi hizi zilitumika katika uchunguzi wa kitaalamu.
Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) iliripoti kuwa Edwin Oduor Odhiambo, anayejulikana pia kama Abdul Rashid, na Dennis Sewe Munyasi walikamatwa siku ya Jumatano na kuwaongoza maafisa hadi nyumbani kwa Odhiambo, ambako silaha zilipatikana.
Wakati huohuo, washukiwa wanne waliohusishwa moja kwa moja na tukio hilo wanazuiliwa na polisi.
Washukiwa wawili muhimu pia walikamatwa Jumatano, na kufanya jumla ya washukiwa walioko kizuizini kufikia kumi.
Mwanasiasa na mfanyabiashara wa Homa Bay, Philip Nahashon Aroko, alihojiwa na maafisa wa DCI Jumatano jioni, ambapo alikana kuhusika na mauaji hayo.
Wakili wake, Danstan Omari, alisema kuwa Aroko alijisalimisha katika Kituo cha Polisi cha Gigiri baada ya kuitwa na DCI.
Polisi pia wanachunguza simu iliyopigiwa msaidizi wa Mbunge wa Were siku ambayo mbunge huyo aliuawa.
Msaidizi huyo, aliyekuwa katika majengo ya Bunge wakati huo, alizungumza na mpigaji simu kwa muda wa dakika moja na sekunde kumi.
Hii haikuwa mara ya kwanza kwa mpigaji huyo kuzungumza na mlinzi wa mbunge huyo.
Siku mbili zilizotangulia, mlinzi huyo alipokea simu kutoka kwa nambari hiyo hiyo.
Wachunguzi wanaamini kwamba simu hii, iliyopigwa saa tano tu kabla ya mbunge kupigwa risasi, inaweza kusaidia kufichua siri ya mauaji hayo.
Vyanzo vilivyo karibu na uchunguzi viliiambia Taifa Leo kwamba nambari hiyo ilisajiliwa siku tatu tu kabla ya mbunge kuuawa. Ilimpigia tu msaidizi huyo wa mbunge.
Chanzo hicho kilisema uchunguzi zaidi wa laini hiyo ulibaini kuwa ilisajiliwa kwa jina la mwanamke kutoka Nyanza ambaye wapelelezi wamebaini tayari alikuwa amekufa wakati kitambulisho chake kilitumiwa kusajili laini hiyo.