• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:55 PM
Bawabu asimulia jinsi mwenzake alivyosombwa na maji Mto Muswii

Bawabu asimulia jinsi mwenzake alivyosombwa na maji Mto Muswii

NA PIUS MAUNDU

BAWABU aliyemtahadharisha mwenzake dhidi ya kuabiri lori kuvuka Mto Muswii uliofurika katika Kaunti ya Makueni, aliaga dunia na kumuacha mwenzake kusimulia kisa hicho.

Wawili hao, Bw Samuel Nzomo na Masila Mulonzi, walikuwa wakielekea nyumbani baada ya kazi kisa hicho kilipotokea.

Hata hivyo, walipofika kwenye mto huo, walipata umefurika na wakalazimika kuungana na mamia ya watu wakiwemo wachuuzi na wafanyabiashara wengine wadogo wadogo ambao pia walitaka kuvuka kuenda kijiji jirani cha Kasikeu.

“Tulikaa kando ya mto kwa zaidi ya saa saba ndipo lori lililokuwa limebeba kokoto lilikuja na kujitolea kuwasaidia waliokwama kuvuka, nilitaka kuungana na wengine kuliabiri lori hilo ila akaniambia nisubiri. Tulisimama tukiangalia lori hilo likivuka na tukafurahia kuona kuwa lilifika upande mwingine salama,” Bw Nzomo aliambia Taifa Leo.

“Lori la pili lilipokuja tukaamua kuliabiri ila likalemewa na sote tukasombwa na mafuriko. Mimi nilibahatika na nikaokolewa ila mwenzangu aliangamia,” akasimulia.

Katika mojawapo ya video ambazo zilinaswa na walioshuhudia, abiria waliokuwa kwenye gari lililozama walionekana wakijaribu kuogelea huku maji yaliyokuwa yanaenda kwa kasi yakiwalemea huku waliokuwa wanatazama wakipiga mayowe.

Hakukuonekana waliojaribu kuwaokoa kwa hofu ya kusombwa pia, wengi wao wakiwaambia kushikilia mti au chochote kile kinachoweza kushikika.

Usafiri katika barabara ya Kasikeu-Sultan Hamud ulikatizwa baada ya mto huo ambao unaanzia katika kaunti jirani ya Kajiado kuvunja kingo zake.

Maafisa wa shirika la Kenya Redcross na Serikali ya Kaunti ya Makueni wabeba mwili ulioopolewa kutoka Mto Kwa Muswii, Kaunti ya Makueni mnamo Aprili 27, 2024. Watu tisa walikufa maji wakijaribu kuvuka mto huo uliofurika wakiwa wameabiri lori. PICHA | PIUS MAUNDU

Bawabu mhanga huyo ni miongoni mwa watu tisa walioaga dunia kwenye ajali hiyo.

“Waliotibiwa na kuruhusiwa kuenda nyumbani ni 14. Tulipokea miili tisa ambapo sita ilikuwa ya wanawake na mitatu ya wanaume,” afisa msimamizi wa hospitali ya kaunti ndogo ya Sultan Hamud, Bi Jane Mwende alisema.

Naibu Gavana wa Makueni Lucy Mulili alisema watu 10 bado haijulikani waliko.

  • Tags

You can share this post!

Gachagua, Sakaja wakabiliana

Polo mjanja apeleka mamanzi kibandani badala ya hotelini

T L