Benki zaweka masharti makali kwa mikopo ‘midogomidogo’
NA KEPHA MURURI
BENKI sasa zimeweka masharti magumu ya kutoa mikopo midogomidogo kama tahadhari baada ya wakopaji wengi kushindwa kulipa mikopo kutokana na uchumi mgumu.
Utafiti mpya uliofanywa na Benki Kuu ya Kenya (CBK) miezi mitatu hadi Desemba 2023, ulionyesha kuwa benki zimekaza na kuongeza masharti kwa mikopo midogo kama njia ya kuzuia kupanda kwa mikopo isiyolipwa.
Haya yanajiri wakati ambapo benki nazo zinatarajia mikopo ya kibinafsi, kwenye samani, bidhaa za nyumba na kibiashara kupanda robo ya mwaka huu unaokamilika mwishoni mwa mwezi huu.
“Kufikia Desemba idadi ya mikopo ambayo haikuwa ikilipwa ilikuwa juu na ilikuwa ikiendelea kupanda. Hali hii haitarajiwi itabadilika kwa sababu sekta mbalimbali bado zinaendelea kufanya vibaya,” ikasema CBK.
Benki nyingi zimekuwa zikitumia mwongozo wa kutoa madeni ambao hasa huzingatia uwezo wa mtu wa kulipa madeni yake na kiasi anachopaswa kuchukua.
Zaidi ya nusu za benki 38 ambazo zina leseni au asilimia 54 za walioshiriki katika utafiti huo walikiri kuwa idadi ya mikopo ambayo haifanyi vizuri inatarajiwa kupanda katika robo ya kwanza ya 2024.
Kukaza huko sheria kwa benki mbalimbali hasa kuhusu mikopo midogo midogo kunajiri wakati ambapo familia nyingi sasa zimerejelea mikopo ili kutimiza mahitaji mbalimbali. Mahitaji hayo ni kama chakula, kodi na mengine madogo madogo ambayo yangekuwa rahisi kutimiza hapo awali kutokana na mishahara yao.
“Kile tunaona ni kuwa wengi hawawezi tena kumudu gharama ya ulipaji wa mikopo. Kuna watu wachache ambao wanakopa kutumia kuwekeza katika miradi mbalimbali,
“Wengi sasa wanakopa pesa ili kutumia kwa mahitaji ya kimsingi badala ya kuzitumia katika miradi kubwa kubwa kama ujenzi wa nyumba au biashara,” akasema Mwenyekiti wa Muungano wa Benki Nchini John Gachora.
Kulingana na takwimu kutoka data ya CBK, kiasi cha mikopo midogomidogo kwa matumizi ya nyumbani ilikuwa Sh524.1 bilioni kufikia Desemba 2023 ikiwa ilipanda kwa asilimia 2.5 mwaka uliotangulia.
Kufikia mwisho wa mwaka uliopita, kiasi cha mkopo ambao haukuwa umelipwa kilifikia Sh621.3 bilioni kutoka Sh635.8 bilioni mnamo Novemba.