Bilionea Devani kuzuiliwa jela siku 13 katika kesi ya mafuta ya ndege
BWANYENYE Yagnesh Devani aliyekwepa kushtakiwa kwa miaka 15 katika kashfa ya Sh7.6 bilioni ya mafuta ya ndege amezuiliwa katika Gereza la Viwandani kwa siku 13 baada ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) kupinga kuachiliwa kwa dhamana.
Hakimu mkuu wa mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Milimani Thomas Nzioki aliagiza Devani afungwe katika gereza hilo baada ya kukwepa kufika kortini kwa miaka 15.
Kibali cha kumtia nguvuni kilitolewa 2009 na alikuwa akisakwa na polisi wa humu nchini na wale wa kimataifa.
Devani aliyetorokea Uingereza 2009 aliwasilisha kesi katika Mahakama Kuu Ulaya akipinga kurudiswa nchini akidai “magereza ya Kenya ni machafu kupindukia.”
Pia alieleza mahakama Uingereza kwamba “hatapata haki katika mahakama za Kenya endapo atarudishwa kufunguliwa mashtaka ya ulaghai wa kiubiki 126,000,000 za mafuta ya ndege ya thamani ya Sh7.6 bilioni.”
Devani alikanusha mashtaka 11 aliyoshtakiwa ya ulaghai wa mafuta ya ndege kiubiki 19,186,130 ambayo kampuni yake Triton Petroleum Company ilidaiwa kuilaghai kampuni ya ng’ambo ya Emirates National Oil Company iliyoko nchini Singapore.
Bw Nzioki aliamuru idara ya urekebishaji tabia imhoji Devani kubaini masuala kadhaa kuhusu tabia yake tangu arudishwe nchini Januari 23, 2024 na kufunguliwa mashtaka mbele ya hakimu mwandamizi Robinson Ondieki.
Pia hakimu aliagiza idara ya urekebishaji tabia ichunguze pasipoti zake.
Na wakati huo huo, Bw Nzioki aliamuru afisi ya DPP ichunguze na kuwasilisha orodha ya wakurugenzi wa Triton kufikia 2009 ili mahakama ijue ikiwa itamwagiza Bw Devani kujibu mashtaka kwa niaba hiyo ya Triton.