Habari za Kitaifa

Bilionea Munga kutimuliwa ardhi ya Delmonte kwa amri ya korti

Na BENSON WAMBUGU July 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Mahakama ya Nairobi imeamuru bilionea mfanyabiashara Peter Munga afurushwe kutoka ardhi ya ekari 75 inayomilikiwa na kampuni ya Del Monte Kenya Limited, iliyoko Kaunti ya Murang’a, kwa kukiuka mkataba wa kuikodisha.

Bw Munga alipata pigo jingine baada ya Jaji wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi, Anne Omollo, kuagiza Shule ya Kimataifa ya Pioneer – taasisi ya kifahari ya elimu inayohusishwa naye – kuondolewa ardhi hiyo.

Jaji Omollo alielekeza kuwa shule hiyo ihamishwe kufikia mwisho wa mwaka huu. Aidha, shule hiyo imepewa hadi Desemba 20, 2025, kukamilisha shughuli zake za masomo bila kutatizwa, kabla ya kuondoka kabisa katika ardhi hiyo.

“Ninazingatia maslahi bora ya mtoto kwa kuruhusu kalenda ya masomo ya mwaka huu ikamilike kabla ya masomo ya wanafunzi kusitishwa,” alisema Jaji Omollo.

Hata hivyo, alielekeza kuwa shule hiyo iendelee kulipa kodi ya kila mwezi kwa Del Monte hadi itakapohama.

Del Monte ililaumu kampuni ya Goshen Gardens Limited kwa kuhamisha mali na mkataba wa kukodisha ardhi hiyo kwa Shule ya Kimataifa ya Pioneer bila kuijulisha, na baadaye taasisi hiyo ikashindwa kulipa kodi, hali iliyosababisha mmiliki wa ardhi kuvunja mkataba.

Kabla ya shule hiyo kuingia, Del Monte ilikuwa tayari imetoa notisi ya kuvunja mkataba wake na Goshen Gardens kwa sababu ya kutolipa kodi.

Del Monte iliwasilisha kesi kortini mnamo 2016, ikitaka miongoni mwa mambo mengine, shule hiyo ifurushwe kutoka ardhi hiyo na kuondoa majengo yote pamoja na mali nyingine.

Mahakama pia iliagiza Kamanda wa Kituo cha Polisi cha Ngati, mjini Murang’a, kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa.

Kwa mujibu wa Del Monte, Goshen Gardens ilikodi ekari 75 za ardhi hiyo kwa miaka minane kuanzia Septemba 3, 2013, kwa kodi ya kila mwezi ya Sh550,000.

Hata hivyo, kufikia Februari 2015, kampuni hiyo ilikuwa imeshindwa kulipa kodi, na ikapewa notisi ya kuhama. Baada ya kuendelea kukaidi malipo, Del Monte ilisitisha mkataba na kuamuru kampuni hiyo kuondoka.

Lakini Goshen Gardens ilishtaki, ikidai Del Monte ilikiuka makubaliano ya mkataba kwa kupunguza ukubwa wa ardhi kutoka ekari 100 hadi 75, na pia kuingia kwenye ardhi hiyo bila idhini, hali ambayo ilisababisha hofu ya usalama ikiwemo kung’olewa kwa ua  shuleni.

Mahakama ilielezwa kuwa Februari 2, 2015, watu wasiojulikana walivamia majengo ya shule hiyo na kuiba mali ya thamani ya Sh1.6 milioni.

Kesi hiyo baadaye ilielekezwa kwa upatanisho, ambapo Goshen Gardens iliruhusiwa kuendelea kutumia ardhi hiyo kwa muda, ikisubiri uamuzi wa mzozo huo.