Billy Mwangi, mwanafunzi aliyetekwa nyara Embu aachiliwa huru, familia yasema
BILLY Munyiri Mwangi, mwanafunzi wa chuo aliyetoweka baada ya kutekwa nyara na wanaume wanne waliovalia barakoa katika mji wa Embu, amepatikana akiwa hai.
Kulingana na familia yake, Mwangi, ambaye alionekana kuwa dhaifu, alifika nyumbani Jumatatu asubuhi na kupelekwa hospitalini kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 24, alitekwa na watu wasiojulikana hadi sasa alipokuwa akisubiri kuhudumiwa katika kinyozi katika mji wa Embu Jumamosi, Desemba 21.
Babake Gerald Karicha mnamo Januari 2 aliambia Mahakama Kuu jijini Nairobi kwamba watekaji nyara wa Mwangi walikuwa wamemfuata kwa siku kadhaa kabla ya kumchukua kwa nguvu.
Gari la watekaji, Karicha alimwambia Jaji Bahati Mwamuye, lilikuwa ni Double Cabin huku lililokuwa likimfuata likiwa aina ya Toyota Fielder la rangi nyeupe nambari za usajili KDG 527 D.
“Mheshimiwa, gari hilo lilikuwa limechunguza nyumba yangu kwa siku tatu. Gari lingine lilikuwa ni Double Cabin ambalo lilikuwa nyuma ya gari aina ya Toyota Fielder,” alisimulia huku akiwa na kilio.
“Walipofika alipo Mwangi, Fielder ilikuwa mbele. Fielder iliondoka mara moja lakini watu wanne, watu wenye nguvu sana walishuka kutoka Double Cabin, wakamvamia mwanangu na kumtupa ndani ya gari. Aliwauliza, nyinyi ni nani, mnanipeleka wapi, wakasema utajulia mbele,” alisimulia Karicha.
Habari zaidi kufuata…