• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Binti ajisalamisha kortini kushtakiwa kwa kughushi wosia wa marehemu babaye

Binti ajisalamisha kortini kushtakiwa kwa kughushi wosia wa marehemu babaye

NA RICHARD MUNGUTI

BINTI wa mmiliki wa kampuni kadha aliyekuwa akisakwa na polisi kwa kughushi wosia alioacha baba yao kwa lengo la kuwalaghai dada zake wawili, alijisalamisha mahakamani Jumanne.

Dinta Devani na mumewe Abhay Singh Pathiana walifika mbele ya hakimu mkuu wa mahakama ya Milimani Bernard Ochoi.

Dinta na Abbay waliandamana na wakili Danstan Omari aliyeomba msamaha kwa niaba yao.

“Dinta na mumewe Abhay hawakujua walikuwa wanatakiwa kufika kortini kujibu mashtaka ya kughushi Wosia wa Balkrishna Harubhai Devani (babaye Dinta) na kurithi baadhi ya kampuni za familia yao,” Bw Omari alidokeza.

Wakili huyo alisema wawili hao walisoma katika mtandao wa Nation.Africa kwamba kibali cha kuwatia nguvuni kimetolewa na hakimu mkuu Bi Susan Shitubi.

Bi Shitubi aliagiza Dinta, Abhay na Addah Nduta Ndambuki wakamatwe kwa kujipatia kwa njia ya ulaghai hisa katika kampuni ya Pelikan Signs Limited.

Kampuni ya Pelikan ndio huandika na kuweka vibao katika barabara kuu zote nchini.

Agizo la kuwatia nguvuni watatu hao lilitolewa wakati mkurugenzi mwingine wa Pelikan Signs Limited, Samuel Ndinguri aliposhtakiwa mbele ya Bi Shitubi. Alikabiliwa na mashtaka matatu ya ulaghai na kujipatia hisa katika kampuni hiyo.

Dinta na Abhay waliomba waachiliwe kwa dhamana kwa “vile polisi hawakuwapa samanzi ya kufika kortini.”

Bw Omari pia alihakikishia mahakama kwamba washukiwa hao watatii maagizo ya mahakama.

Kiongozi wa mashtaka hakupinga ombi la Dinta na mumewe kuachiliwa kwa dhamana ila aliomba hakimu awaamuru wafike katika kituo cha polisi cha Parklands kuchukuliwa alama za vidole.

“Washukiwa hawa hawajachukuliwa alama za vidole hivyo naomba wafike mbele ya afisa anayechunguza kesi hii kuchukuliwa kisha warudi kortini Alhamisi kujibu mashtaka,” kiongozi wa mashtaka Bw James Gachoka aliomba.

Akitoa uamuzi Bw Ochoi aliwaachilia washtakiwa hao kwa dhamana ya Sh100,000 pesa taslimu kila mmoja.

Wanatarajiwa kujibu mashtaka manane dhidi yao.

  • Tags

You can share this post!

Vituo vya petroli vinavyoogelea maji ya mafuriko vifungwe...

Octopizzo: Wasanii wa sasa hawatoboi kisa Insta na TikTok

T L