Bodaboda waweka hofu sekta ya uchukuzi kwa mtindo wa kuchoma magari
WAHUDUMU wa boda boda katika sehemu mbalimbali nchini wamekuwa wakichukua sheria mikononi mwao kwa kuteketeza magari na kusababisha hasara ya thamani kubwa.
Ndani ya wiki moja iliyopita visa vitatu kama hivyo vimeripotiwa katika mtaa wa Makongeni, Thika, mji wa Luanda Kaunti ya Vihiga na katika barabara kuu ya Thika, karibu na mji wa Juja.
Mnamo Jumapili rabsha zilizuka Makongeni, Thika baada ya wahudumu wawili kupigwa risasi na afisa mmoja wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI).
Wakilipiza kisasi, wahudumu wa bodaboda waliojawa na hasira walijitokeza kwa wingi na kuziba barabara kabla ya kuliteketeza gari la afisa huyo, aina ya Audi.
Katika mji wa Luanda magharibi mwa Kenya, wahudumu wa bodaboda kwa mara nyingine walipandwa na hamaki kuteketeza matatu moja iliyodaiwa kumgonga na kumuua mwenzao mmoja.
Kisa sawa na hicho kilitokea katika barabara kuu ya Thika pale basi la kampuni ya Super Metro lilipoteketezwa baada ya kuhusika katika ajali iliyochangia kifo cha mwendeshaji bodaboda.
Abiria waliokuwa wakisafiri kwa basi hilo waliponea bila kujeruhiwa lakini usimamizi wa kampuni hiyo ulipata hasara ya mamilioni ya pesa.
Chama cha Wahudumu wa Vyombo vya Uchukuzi wa Umma (MMOA), kikiongozwa na Katibu Mkuu, Bw Wilfred Bosire, kimelaani visa hivyo kikivitaja kama uvunjaji wa sheria na tishio kwa sekta ya uchukuzi nchini.
“Vitendo kama hivi vya uvunjaji wa sheria havifai kuruhusiwa kutokea. Ni uhuni mkubwa kwa watu fulani kuteketeza magari yanayowahudumia maelfu ya watu na yanayochangia pakubwa ufanisi wa sekta ya uchukuzi. Watu kama hao wanafaa kuchukuliwa hatua kali za kisheria,” akasema katibu mkuu wa MMOA, Bw Wilfred Bosire.
Aliwashutumu maafisa wa usalama kwa kusalia kimya huku uhayawani huo ukiruhusiwa kuendelea.
“Ndani ya wiki moja, tumeshuhudi visa vitatu vya magari kuteketezwa. Lakini inashangaza kuwa hatujaona taarifa kutoka kwa Inspekta Jenerali wa Polisi, Waziri wa Usalama na Idara ya DCI. Hamna mshukiwa hata mmoja amenaswa kuhusiana na visa hivyo vya uvunjaji sheria,” Bw Bosire akaeleza.
Kiongozi huyo wa MMOA alionya kuwa ikiwa serikali itafeli kuchukua hatua, wahudumu wa magari ya uchukuzi watalazimika kukodi walinzi wa magari yao na abiria wao.
“Tunatoa nafasi kwa Inspekta Jenerali wa Polisi kushughulikia changamoto hii. La sivyo, hatutakuwa na jingine ila kama wahudumu tutajitafutia walinzi wetu barabarani,” Bw Bosire akaonya.
Alipuuzilia mbali madai ya baadhi ya wahudumu wa bodaboda kwamba vitendo vyao ni njia mojawapo ya kujikinga baada ya ajali kutokea.
“Yeyote anayesema hivyo ni mhalifu. Hamna mtu aliye na kibali cha kutekeleza uhalifu ndani ya nchi hii,” Bw Bosire akasema.