Bomet yapitisha bajeti inayotenga Sh5 milioni kumwonyesha Rais ‘ukarimu’ anapozuru
BUNGE la Kaunti ya Bomet limeidhinisha bajeti ya Sh9.7 bilioni ya Mwaka wa Kifedha wa 2024-2025, ambayo inajumuisha Sh5 milioni kwa ziara za Rais katika eneo hilo, licha ya hafla kama hizo kugharamiwa na serikali ya kitaifa.
Bajeti hiyo imeibua hisia tofauti miongoni mwa wakazi wa Bomet.
Pesa hizo zinakusudiwa kugharamia ziara za rais, ikiwa ni pamoja na za Mke wa Rais, Naibu Rais, na Mke wa Naibu wa Rais, hasa kutokana na kasumba ya awali kuhusu ukarimu wa kaunti wakati wa ziara hizo.
“Ziara ya Rais inajumuisha Rais, Mke wa Rais, Naibu Rais, na Mke wake. Serikali ya kaunti inaendesha mipango na afisi ya Mke wa Naibu Rais,” ilisema stakabadhi ya bajeti ya 2024-2025 iliyowasilishwa kwenye bunge la kaunti.
Bajeti hiyo imeidhinishwa licha ya hatua za Rais kutaka uadilifu katika masuala ya fedha.
Aidha, inaongeza kwamba kulingana na uzoefu wa miaka iliyopita, kaunti kuwa mwenyeji wa rais aliyetembelea kaunti kwa siku tatu akiambatana na mkewe, inafaa kupanga bajeti ya kumpokea rais na masuala mengine.
“Mradi wa upanzi wa miti katika eneo la Chepalungu unazidi kupokea wageni wa hadhi ya juu na una uwezekano wa kuvutia ziara za Rais kulingana na shughuli zilizopendekezwa, hivyo kuna haja ya kuongeza bajeti (kwa Sh1 milioni kutoka Sh4 milioni za awali),” kaunti inasema katika bajeti.
Kuidhinishwa kwa bajeti hiyo kunajiri licha ya hatua za kubana matumizi alizotangaza Rais William Ruto kuzitaka taasisi za serikali ya kitaifa na kaunti kupunguza matumizi.