Bonge la kazi kwa Wetang’ula bunge likirejelea vikao
BUNGE la Kitaifa Jumanne, Septemba 23, 2025 lilianza tena vikao vyake baada ya mapumziko marefu, huku Spika Moses Wetang’ula akitarajiwa kuiongoza kufanya maamuzi yanayotarajiwa kutoa mwelekeo wa taifa katika miezi ijayo.
Katika kipindi hiki ajenda ya Bunge imejaa masuala nyeti, yakiwemo miswada zaidi ya 12 ya kipaumbele, hoja za kisiasa, karatasi za sera, na mageuzi ya kiuchumi na kiutawala.
Kwa Wetang’ula, aliye na tajriba ya zaidi ya miongo minne katika utumishi wa umma, jukumu lake ni kuongoza Bunge katika mijadala migumu, huku akiendeleza misingi ya demokrasia, usawa na uwajibikaji.
“Tunaporejelea vikao vyetu baada ya mapumziko marefu, nawahimiza Wabunge wote wakumbatie moyo wa kuhudumu, na wasimame imara kama walinzi wa matumaini ya Wakenya. Taifa halitazami Bunge hili kwa kelele, bali kwa suluhu; si kwa migawanyiko, bali kwa umoja; si kwa visingizio, bali kwa matokeo. Hebu tuunde sheria kwa heshima, tupige msasa kwa ujasiri, na tuwakilishe kwa uadilifu, kwani historia haitatutathmini kwa maneno tunayosema, bali kwa huduma tunayotoa kwa Kenya,” Bw Moses Wetang’ula aliambia wabunge.
Miongoni mwa mambo ya kwanza ya kujadiliwa ni uteuzi wa mabalozi, na viongozi wa taasisi nyeti kama Tume ya Haki za Kibinadamu na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa.
Spika pia ataongoza mijadala kuhusu sera kama mpango wa kubinafsisha Kampuni ya Mabomba ya Mafuta (KPC), makubaliano ya kibiashara na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), na mkataba wa kuondoa ushuru maradufu kati ya Kenya na Singapore.
Kwa upande wa wananchi wa kawaida, Wetang’ula atasimamia mjadala kuhusu Mswada wa Marekebisho ya Ajira unaopendekeza haki ya mfanyakazi kupumzika bila kuingiliwa na mawasiliano ya kikazi baada ya saa za kazi.
Pia, Bunge litajadili Mswada wa Ugavi wa Fedha kwa Kaunti, pamoja na miswada mingine inayohusu sekta ya kahawa, usimamizi wa maafa, rasilmali asilia na ujasiriamali wa vijana.
Katika kuimarisha utawala bora, Spika Wetang’ula atakuwa na jukumu la kuratibu mjadala kuhusu uhusiano kati ya Bunge la Kitaifa na Seneti, suala ambalo limezua migogoro ya mara kwa mara.
Aidha, Bunge litaangazia mswada wa barabara unaopendekeza ugatuzi kamili wa barabara za kaunti, pamoja na mswada wa ubinafsishaji wa mashirika ya umma ili kuongeza ufanisi na uwazi.
Wetang’ula, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Maspika wa Afrika Mashariki, anaendeleza diplomasia ya Bunge kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa kama CPA, PAP na EALA.
Huku michezo ya mabunge ya EALA yakitarajiwa kufanyika Uganda mwezi Desemba, Kenya inatarajiwa kuonyesha nguvu zake za kisiasa na kidiplomasia kupitia uhusiano wa mabunge.
Akisisitiza kwamba viongozi ni watumishi wa wananchi, Spika Wetang’ula anasema ataendelea kuwa “mtumishi wa wananchi, si bwana wao.”