Habari za Kitaifa

Bunge la Amerika kuamua hatima ya spika anayeandamwa na mbunge wa chama chake

May 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WASHINGTON DC, AMERIKA

NA MASHIRIKA

WABUNGE wa Amerika wanatarajiwa kupiga kura wiki ijayo, kutathmini hoja ya kumwondoa mamlakani Spika wa Bunge Bw Mike Johnson, baada ya mbunge wa chama chake cha Republican kuwasilisha hoja ya kumtaka ajiuzulu Jumatano, kwa kusaliti chama na kukiuka kanuni ambazo huenda zikasababisha mizozo ya kisiasa kwenye uchanguzi wa Novemba.

Mbunge wa chama cha Republican Bi Marjorie Taylor Greene alisema atashinikiza wanachama wenza kupiga kura hiyo ya kumtimua spika huyo baada ya viongozi wa chama cha Democratic kutangaza kuwa watapiga kura za kuokoa nafasi ya spika wa chama cha Republican.

Bi Greene ambaye alikuwa akiongea nje ya Ikulu, alikashifu viongozi wa Chama chake walio kwenye ngazi za juu kwa kusukuma maslahi yao ya kibinafsi kinyume na maombi ya wafuasi, ikiwa ni pamoja na kutoka kwa Donald Trump, ili kuepusha mzozo mwingine wa kisiasa kwenye uchaguzi wa Novemba.

“Tunahitaji viongozi katika Baraza la Wawakilishi ambao watafanya hili. Bw Mike Johnson hawezani na kazi hiyo,” alisema Bi Greene.

“Kila mjumbe wa Congress anahitaji kupiga kura hiyo na kuhakikisha anaondolewa,” aliongeza Bi Greene.

Malumbano hayo yanahatarisha kuhifadhi udhibiti wa Republican katika bunge. Awamu mpya ya machafuko huenda yakashuhudiwa kwani wabunge wenye vyeo watalazimika kuchangua kati ya kumwondoa Spika Johnson au kujiunga na Wanademocratic ili aendelee na kazi.

Katika taarifa yake Bw Johnson, alisema hatua ya Bi Greene si sawa kwa wanachama wa Republican, taasisi na nchi.

Wanachama wa Democratic, wanaona Bw Johnson kuwa mshirika aliye shupavu na tayari anaweza kuongoza chama chake cha Republican bila kusikiza sauti zinazozuia ajenda ya kawaida ya serikali, ikiwa ni pamoja na kufadhili serikali kwa kuunga mkono Ukraine na washirika wengine wa Amerika nje ya nchi.

Kiongozi wa Democratic, ambaye pia ni mwakilishi wa jimbo la New York Bw Hakeen Jeffries akiwa na kundi lake, walitoa taarifa ya kusema kuwa ni wakati wa kufungua ukurasa mwingine kuhusiana na malumbano yanayoendelea. Bw Jeffries alitangaza kuwa watahakikisha wameangusha mswada wa Bi Greene ambao ni jaribio la kumwondoa spika.

“Kwanzia mwanzo, chama cha Republican kimekuwa kikikumbwa na mizozo, kutofanya kazi na kuwa na itikadi kali kwa wananchi wa Amerika,” alisema Bw Jeffries.

Bw Johnson amekuwa spika tangu Oktoba 2023, na anakabiliwa na tishio la kuondoka kwenye chama chake.