Bunge la ‘waheshimiwa’ lilivyokosewa heshima na kufanyiwa uharibifu ulioacha wengi vinywa wazi
KUVAMIWA kwa Bunge kulikofanyika saa ile ile wakati uharibifu mkubwa ulikuwa unafanyika katika afisi za wabunge kulikuwa jambo ambalo halijawahi kufanyika katika historia ya nchi hii.
Inabidi kurudi nyuma miaka 117 iliyopita hadi wakati Bunge la Kenya lilianza kuhisi staha ya hali ya juu kwa jinsi majengo na mandhari yake yalikuwa. Wakati huo bunge lilikuwa linaitwa Baraza la Sheria (Legislative Council) au LegCo na lilikuwa katika barabara ya Haile Selassie.
“Muundo wa majengo ya Bunge, heshima, taadhima, mavazi ya Spika na ya wabunge, taratibu za shughuli ziliundwa kuashiria heshima kubwa, na ndio maana hata wakaitwa “waheshimiwa”,” kinasema kitabu cha historia ya Bunge.
Lakini jana, Bunge ambalo lilianza vikao vyake 1907 lilivamiwa na walalahoi ambao ni kinyume kikubwa na walalahai ambao hutumia muda mwingi kufanya kazi, kula, na kubarizi humo.
Vijana waliokuwa wamegadhabishwa na kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2024 hawakuona lolote la heshima huko walipovamia na kufanya uharibifu ya kushtukiza.
Huku hayo yakifanyika, wabunge ambao walikuwa wameshiriki kupitisha mswada huo tatanishi walikuwa wanawindwa katika sehemu nyingi nchini.
Mbunge wa Molo Kuria Kimani, Kimani Ichungw’ah (Kikuyu), Oscar Sudi (Kapseret), Njoroge Wainaina (Kieni, Zaheer Jhanda (Nyaribari Chache, Emathe Namuar (Turkana Kati) David Gikaria (Nakuru Mashariki), Samuel Arama (Nakuru Magharibi) na Paul Chebor (Rongai) walikuwa miongoni mwa wabunge ambao makazi kibinafsi, biashara au afisi ziliwindwa.