Habari za Kitaifa

Bungei, aliyelaumiwa na Gen Z kwa ukatili wakati wa maandamano, ahamishwa

Na KAMORE MAINA December 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKATI wa kilele cha maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha mnamo Julai 20, 2024, aliyekuwa Mkuu wa Polisi Nairobi, Adamson Bungei, alimulikwa vikali na umma.

Kwa upande wa Serikali, Bw Bunge alichukuliwa kama mtu aliyetarajiwa kurejesha amani huku waandamanaji wa kizazi cha Gen Z wakijaa barabarani.

Hata hivyo, kwa mashirika ya haki za binadamu, alikuwa mkuu wa polisi aliyekuwa hatari, aliyesimamia ukatili mkali wa waandamanaji waliodumisha amani.

Mamia ya waandamanaji wa Gen Z  walijaa mitaa ya Nairobi wakidai kuondolewa kwa Mswada wa Fedha, ambao walidai ungeongeza mzigo kwa walipa kodi.

Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK) kilimlaumu Bungei na maafisa wake kwa jinsi walivyoshughulikia maandamano hayo.

Bw Bungei ni miongoni mwa makamanda wakuu wa polisi wa Nairobi waliotakiwa kufika kortini kutoa ufafanuzi kuhusu vifo vya waandamanaji, wakiwemo Rex Masai, aliyekufa baada ya kupigwa risasi wakati wa maandamano.

Katika ushahidi wake, alisema kuwa hawezi kusema jinsi Masai alivyopoteza maisha na amekanusha madai kuwa waandamanaji huyo alipigwa risasi na polisi.

Mnamo Januari 16, 2025—miezi mitano baada ya ukatili huo Bungei hakuhamishwa kutoka Nairobi, bali pia alipandishwa cheo na kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Operesheni za Polisi katika Vigilance House.

Alipandishwa cheo hadi Msaidizi Mkuu wa Inspekta Mkuu wa Polisi (SAIG), akisimamia operesheni zote za polisi nchini na kupata nafasi muhimu katika urithi wa uongozi wa polisi.

Kwa mtu ambaye alitumia sehemu kubwa ya kazi yake katika Polisi wa Utawala kabla ya kuhamia polisi wa kawaida, cheo chake kipya na ofisi yake vilimfanya kuwa mmoja wa makamanda wenye mamlaka makubwa zaidi katika Vigilance House.

Alikuwa afisa wa tatu kwa utaratibu wa uongozi wa polisi.

Hata hivyo, Alhamisi—miezi nane tu baada ya kuchukua jukumu la operesheni—Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja alitangaza mabadiliko madogo ya uongozi, na kumhamisha tena Bw Bungei.

Sasa anahamia Bruce House kuongoza Kitengo cha Kitaifa cha Silaha Ndogo, idara iliyo chini ya Ofisi ya Rais inayosimamia jitihada za kupunguza silaha haramu.

Anachukua nafasi ya Jecinta Muthoni, ambaye anatarajiwa kustaafu mwishoni mwa mwezi.