• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 11:29 AM
Bwanyenye adinda kufika kortini kujibu kesi ya wizi wa mafuta ya ndege

Bwanyenye adinda kufika kortini kujibu kesi ya wizi wa mafuta ya ndege

NA RICHARD MUNGUTI

BWANYENYE Yagnesh Mohanlal Devani Jumatatu, Aprili 15, 2024 alikosa kufika kortini kwa mara ya tatu mfululizo wakati wa kusikizwa kwa kesi inayomuandama ya ulaghai wa mafuta ya ndege yenye thamani ya Sh1.5 bilioni miaka 16 iliyopita.

Devani aliyekuwa ametorokea Uingereza kukwepa kushtakiwa alirudishwa humu nchini mapema mwaka huu, 2024, baada ya jitihada zake kupinga kushtakiwa nchini kwa ulaghai huo kugonga mwamba.

Mahakama Kuu ya Uingereza ilitupilia mbali ombi la mfanyabiashara huyo kupinga kurudishwa Kenya kujibu mashtaka.

Januari 2024, Devani aliyetiwa nguvuni na polisi wa kimataifa -Interpol- alirudishwa nchini na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga na kushtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi Robinson Ondieki katika Mahakama ya Milimani.

Kesi yake ilipotajwa Devani hakuwa amefika kortini lakini Wakili Moses Kurgat anayemtetea aliwasilisha ombi mshtakiwa aruhusiwe kutofika kortini wakati wa kutajwa kwa kesi hiyo.

Lakini Kurgat hakueleza aliko Devani na sababu za kutaka asifike mahakamani.

Kiongozi wa mashtaka Eliphaz Ombati alieleza mahakama hajakabidhiwa nakala ya ombi la mshtakiwa la kuomba aruhusiwe kutofika kortini.

Mahakama ilimwamuru Wakili Kurgat amkabidhi Bw Ombati nakala ya ombi hilo.

“Ombi hili la Devani litasikizwa Aprili 29,2024. Mkabidhi Bw Ombati nakala ya ombi hilo,” Bw Ondieki aliamuru.

Devani alikana kulaghai Benki ya Kenya Commercial (KCB) zaidi ya Sh1.5 bilioni kwa kuuza mafuta ya ndege katika kituo cha Kipevu Mombasa.

Mshtakiwa kupitia kampuni yake ya Triton aliuza mafuta hayo aliyokuwa amenunua na pesa za KCB kinyume cha maagano na benki hiyo.

Vibali viwili vya kumkamata Devani havijafutiliwa mbali. Polisi wanaendelea kumsaka

 

  • Tags

You can share this post!

Afisa wa polisi anayetaka apewe kazi ya kuhubiria wenzake...

Wakenya wataka bei ya gesi ipunguzwe baada ya stima kushuka...

T L