Habari za Kitaifa

Caroli Omondi amtaka Raila akome kuingilia siasa za Kenya kuanzia sasa  

April 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA GEORGE ODIWUOR

MBUNGE wa Suba Kusini Caroli Omondi sasa anamtaka Kiongozi wa Azimio la Umoja, Raila Odinga akome kushiriki siasa za humu nchini baada ya kutangaza azma ya kuwania uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC).

Bw Omondi alisema kuondoka kwa Raila katika siasa za Kenya kutasababisha kuwe na ushindani sawa katika eneo la Luo Nyanza.

Bw Odinga anajivunia umaarufu mkubwa eneo hilo na wagombea anaowaidhinisha hushinda kwa urahisi.

Bw Odinga mwenyewe amenukuliwa akisema kuwahi kazi ya AUC haitamzuia kutoa kauli yake kuhusu masuala yanayoathiri nchi hasa sera za serikali.

Kuhusu siasa za Luo Nyanza, Bw Odinga hivi majuzi alimuidhinisha Mbunge Mteule John Mbadi kutwaa kiti cha Suba Kusini kutoka kwa Bw Omondi mnamo 2027.

Bw Omondi ni kati ya wabunge wa ODM ambao walikiasi chama na kuamua kufanya kazi na utawala wa Kenya Kwanza baada ya kura ya 2022.

Akizungumza katika uwanja wa Nyakiamo, mjini Sindo, wikendi, Bw Omondi alisema wanasiasa ambao wamekuwa wakitegemea kuidhinishwa na Raila watabaki mayatima mnamo 2027.

Akiwa uga wa Nyankiamo, Bw Omondi alitoa mabasi matatu kwa shule ya upili ya Nyabera na zile za mseto za Nyagwethe na Gingo.

Pia alisambaza hundi za basari zenye thamani ya Sh40 milioni kwa wanafunzi kutoka familia maskini.

“Wakati umewadia ambapo wanasiasa wanastahili kuchaguliwa kulingana na rekodi yao ya maendeleo. Raila akienda AU hatasumbuliwa na wanasiasa ambao humtaka awaidhinishe hapa Nyanza,” akaongeza.