Habari za Kitaifa

CDF: Jenerali Kahariri ndiye mkuu mpya wa majeshi

May 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MWANDISHI WETU

RAIS William Ruto amempandisha cheo Luteni Jenerali Charles Muriu Kahariri kuwa Jenerali na kisha kumteua kuwa Mkuu wa Majeshi (CDF) kufuatia kifo cha Francis Ogolla.

Naye Meja Jenerali Fatuma Gaiti Ahmed kwenye mabadiliko mapya, amepandishwa cheo kuwa Kamanda wa Jeshi la Wanahewa na kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza kitengo chochote katika jeshi.

Jenerali Kahariri anajaza nafasi ya Ogolla ambaye pamoja na wanajeshi wengine tisa, waliaga dunia kufuatia ajali ya helikopta yao katika eneo la Sindar, Kaunti ya Elgeyo Marakwet mnamo Aprili 18, 2024.

Mnamo Machi 2024 Dkt Ruto alimpandisha cheo Kahariri, wakati huo akiwa Meja Jenerali, kuwa Luteni Jenerali na Naibu Mkuu wa Majeshi (VCDF). Hii ilifuatia kustaafu kwa aliyekuwa VCDF wakati huo, Jenerali Jonah Mwangi na Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu Luteni Jenerali Peter Mbogo baada ya wawili hao kufikisha umri hitajika.

Meja Jenerali David Kimaiyo Tarus ndiye Kamanda wa kikosi cha Wanajeshi wa Nchi Kavu.

Kwenye mabadiliko hayo ya mnamo Machi, Kamanda wa Kikosi cha Jeshi la Wanamaji, Meja Jenerali Jim Mutai alipandishwa cheo hadi kuwa Luteni Jenerali na kuteuliwa kuwa Naibu Chansela wa Chuo cha Kitaifa cha Mafunzo ya Ulinzi.

Ni mabadiliko yaliyoidhinishwa kwenye mkutano wa Baraza la Idara ya Ulinzi chini ya uenyekiti wa Waziri wa Ulinzi Aden Duale.

Rais ndiye Amiri Jeshi Mkuu.