Habari za Kitaifa

Chaguzi ndogo 24 kufanyika mwaka huu – IEBC

Na COLLINS OMULO August 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetangaza kuwa chaguzi ndogo zote 24 za viti mbalimbali zitafanyika kabla ya mwisho wa mwaka huu, huku ikisisitiza kuwa uchaguzi mkuu ujao utafanyika mwezi Agosti mwaka 2027 kama ilivyopangwa.

Tangazo hili limejiri wakati ambapo tume hiyo imekanusha madai kuwa kuna njama fiche za “kuiba” kura katika uchaguzi mkuu ujao, ikisema kuwa chaguzi nchini Kenya husimamiwa kwa sheria madhubuti na hivyo hakuna nafasi ya udanganyifu.

Akizungumza katika kikao na wadau wa vyombo vya habari jana, Mwenyekiti wa IEBC, Bw Erastus Ethekon, alisema Kamati ya Usimamizi wa Uchaguzi ya tume hiyo inakamilisha ratiba ya chaguzi hizo ndogo, na itatolewa rasmi wiki ijayo.

“Tutatangaza ratiba ya chaguzi ndogo katika muda wa wiki moja, na tumepanga kuzimaliza zote kabla ya mwisho wa mwaka huu,” alisema Bw Ethekon.

Aliongeza kuwa kamati hiyo inafanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha muda wa kikatiba unazingatiwa katika kutekeleza chaguzi hizo.

Bunge linatarajiwa kutoa ilani mpya za kutangaza viti saba vya ubunge vilivyo wazi, hatua ambayo itafanya tume kuandaa chaguzi ndogo.

Baadhi ya maeneo hayo hayajakuwa na wawakilishi waliochaguliwa kwa zaidi ya miaka miwili tangu viti hivyo kuwa wazi.

Bw Ethekon alifafanua kuwa ilani za awali za kutangaza viti kuwa wazi zilikuwa zimeisha muda wake kwa kuwa tume haikuwa imeundwa upya kufuatia kuondoka kwa makamishna wa awali mnamo Januari 2023.

Viti vya ubunge vilivyo wazi ni Ugunja (baada ya Opiyo Wandayi kuteuliwa Waziri wa Kawi na Petroli), Kasipul (baada ya kuuawa kwa Mbunge Ong’ondo Were mwezi Aprili), Mbeere Kaskazini (Geoffrey Ruku aliteuliwa kuwa Waziri wa Huduma kwa Umma), Banisa (Mbunge Hassan Kullow alifariki katika ajali ya barabarani Machi 2023), Magarini (Mahakama ya Juu ilibatilisha ushindi wa Harrison Kombe) na Malava (Mbunge Malulu Injendi alifariki Februari 2025).

Kiti cha Seneta Baringo (Seneta William Cheptumo alifariki Februari 2025).

Tafsiri: BENSON MATHEKA