Chaguzi za Novemba 27 mtihani kwa Kenya Moja
CHAGUZI ndogo zijazo zitakazofanyika Novemba 27 mwaka huu zimetajwa kama mtihani mgumu kwa wabunge wa vuguvugu la Kenya Moja.
Vuguvugu hilo linaleta pamoja waasi wa mirengo ya kisiasa ya Raila Odinga na Rigathi Gachagua, kwa lengo la kubuni muungano wa kuzima ndoto ya Rais William Ruto kushinda muhula wa pili.
Katika chaguzi hizo wapigakura Baringo watajitokeza kumchagua seneta mpya kujaza nafasi iliyoachwa wazi kufuatia kifo cha William Cheptumo hapo Machi 25 mwaka huu.Nao wapigakura katika maeneobunge ya Banissa, Kasipul, Magarini, Malava, Ugunja na Mbeere Kaskazini pia watachagua viongozi wapya.Isitoshe, wapigakura katika wadi 18 watachagua wawakilishi (MCAs) wapya.
Miongoni mwa wadi hizo ni Angata Nanyokie katika kaunti ya Samburu, Chemundu/Kapng’etuny (Nandi), Narok Mjini (Narok), Purko (Kajiado), Tembelio (Uasin Gishu), wadi za Nyansiongo, Nyamaiya na Ekerenyo zilizo Kaunti ya Nyamira, wadi za Lake Zone na Nanaam zilizo Kaunti ya Turkana.
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) tayari imetangaza kipindi cha kampeni kitakachoanza Oktoba 8 hadi Novemba 24, huku orodha ya wagombeaji ikihitajika kuwasilishwa ifikapo Septemba 17.
Kulingana na mchanganuzi Festus Wangwe, chaguzi hizo zinawahusu viongozi wa vuguvugu la Kenya Moja kwa sababu vyama vyao vinashiriki.“Kwa mfano kiongozi wa Kenya Moja Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna ni Katibu Mkuu wa ODM inayodhamani wagombeaji katika viti kadhaa katika ngome zake za Nyanza, Pwani na Kakamega.
Sasi inasubiriwa kuonekana ikiwa atajitokeza kuwafanyia kampeni wagombeaji wa ODM ilhali chama hicho kinashirikiana na Rais Ruto. Hii ni kwa sababu Sifuna haungi mkono serikali jumuishi wala azma yake ya kutaka kuhudumu miaka mitano zaidi hadi 2032,” anasema.
“Kwa mfano, juzi akiwa Siaya, Rais Ruto alitangaza kuwa chama chake cha UDA kitaunga mkono ODM katika chaguzi ndogo za Ugunja, Kasipul na Magarini. Kwa upande mwingine ODM imeonyesha nia ya kuunga mkono wagombeaji wa UDA katika uchaguzi mdogo wa useneta wa Baringo na chaguzi katika maeneo bunge Malava na Mbeere Kaskazini,” Bw Wangwe anasema.
Kulingana na uchanganuzi huyo inasubiriwa kuonekana kiwa Bw Sifuna, kama Katibu Mkuu wa ODM ataendesha kampeni ya kupinga wagombeaji watakaoungwa mkono, kwa pamoja, na chama chake na kile cha UDA, kuendeleza upinzani wake dhidi ya serikali jumuishi.
Kwenye mahojiano katika runinga moja ya humu nchini mapema mwezi jana, Bw Sifuna alisema “hamna serikali jumuishi, serikali iliyoko ni ile ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais mwenye mamlaka ya kuteua mawaziri wakiwemo wale kutoka ODM.”
Bw Sifuna alishikilia kuwa “ODM inasalia chama huru chenye maadili yake na inayoendesha shughuli zake kwa lengo la kuunda serikali kivyake au kwa kushirikiana na vyama vyenye maono sawa na yake.
“Washirika wenye maoni sawa hawawezi kujumuisha wale wanaoendeleza ubakaji na mauaji ya raia wasio na hatia, kushiriki ufisadi na kuendeleza ulagha.” Sifuna akaeleza akionekana kurejelea uongozi wa Kenya Kwanza.Baadhi ya wachanganuzi wamedai kuwa kauli za Seneta Sifuna zinaakisi misimamo ya Bw Odinga ikizingatiwa kuwa mara sio moja Waziri huyo
Mkuu wa zamani amejitokeza akitetea kila anachosema ni “haki ya Sifuna kutoka kauli zake kwa bila kudhibitiwa.”Kulingana na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa John Okumu, chaguzi ndogo zijazo zinatarajiwa kubaini uhalisia wa mambo kuhusu msimamo wa Sifuna.
Kwa upande mwingine, chaguzi hizo ndogo zitaonyesha msimamo kamili wa kisiasa wa Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba, ambaye pia ni mwanachama wa Kenya Moja.
Kulingana na Profesa Peter Kagwanja chaguzi ndogo zijazo zitamwanika mbunge huyu ikizingatiwa kuwa anatoa eneo ambalo ni ngome ya Bw Gachagua.“Kwa mfano, itabainika ikiwa Bi Wamuchomba atamuunga mkono au kumpinga mgombea wa DCP katika eneo bunge la Mbeere Kaskazini,” akaeleza.