• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:55 AM
Chelogoi aonywa dhidi ya kuingiza siasa katika kesi

Chelogoi aonywa dhidi ya kuingiza siasa katika kesi

NA RICHARD MUNGUTI

ONYO kali limetolewa dhidi ya aliyekuwa naibu mkuu wa mkoa wa Nairobi Davis Nathan Chelogoi kwamba atajua kilichomtoa kanga manyoya endapo ataingiza siasa katika kesi inayomkabili ya ulaghai wa shamba la ukubwa wa hekta 7.390 lenye thamani ya Sh1.35 bilioni.

Hakimu Mwandamizi Bi Dolphina Alego alimweleza Chelogoi wazi wazi “nitafutilia mbali dhamana hii ya Sh2.5 milioni pesa taslimu ninayokupa endapo utaendelea kuzungumza kuhusu kesi hii katika vyombo vya habari.”

Bi Alego alisema amesoma katika vyombo vya habari na pia akaonyeshwa picha ya wakili Brian Asa anayemwakilisha Bw Chelogoi akiwa na mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa wakijadili suala hilo la shamba hilo ambalo umiliki wake umezua tumbojoto.

Mbali na Bw Chelogoi pia mlalamishi Ashok Shah alionywa dhidi ya kuwaomba wanasiasa wenye ushawishi mkuu kumsaidia asipokonywe shamba hilo.

Hakimu alimuonya Bw Chelogoi, mwenye umri wa miaka 72 kwamba “sitakuwa na budi ila kumsukuma gerezani akizugumzia kuhusu shamba hilo katik vyombo vya habari.”

Bi Alego alitoa tahadhari hiyo alipompunguzia dhamana Chelogoi kutoka Sh5 milioni hadi Sh2.5 milioni baada ya kusema ameshindwa kabisa kupata dhamana aliyopewa ya Sh10 milioni ama pesa taslimu Sh5 milioni.

Hakima alimruhusu bintiye Chelogoi na rafiki wa familia yao kumsimamia dhamana.

“Mtahakikisha Bw Chelogoi amefika kortini Aprili 9, 2024, wakati wa kusikilizwa kwa kesi hii. Endapo hatafika kortini kuendelea na kesi, basi ninyi mtasukumwa ndani pia,” alionya hakimu.

Bw Chelogoi ambaye tangu Alhamisi wiki jana amekuwa katika gereza la Industrial Area, alieleza mahakama hakupata pesa za kugharimia matibabu katika Nairobi Hospital alipokuwa ameagizwa alazwe.

Bw Chelogoi alipelekwa hospitali na maafisa wa idara ya magereza baada ya kupewa dhamana ya Sh10 milioni katika kesi ya ulaghai wa shamba la Sh1.35 bilioni.

Hakimu mwandamizi Dolphina Alego aliamuru mshtakiwa apelekwe Nairobi Hospital baada ya kufahamishwa “hakupata matibabu katika Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) kufuatia mgomo wa madaktari ambao umeingia wiki ya tatu.”

Hakimu alifahamishwa na wakili Prof Tom Ojienda kwamba Bw Chelogoi aliugua Ijumaa alipokuwa katika gereza la Viwandani alipopelekwa Alhamisi wiki iliyopita baada ya kukana mashtaka nane ya ulaghai wa shamba la wafanyabiashara Ashok Rupshi Shah na Hitenkumar Raja.

Bi Alego alielezwa ni shamba la ukubwa wa hekta 7.390 na la thamani ya Sh1,350,000,000.

Mahakama ilielezwa shamba hilo liko eneo la Lower Kabete.

Akiwasilisha ombi kwamba Bw Chelogoi apelekwe Nairobi Hospitali, Prof Ojienda alisema: “Mshtakiwa alipelekwa KNH lakini hakupokea matibabu na wala hakulazwa kufuatia mgomo wa madaktari.”

Alisema daktari wake alimtembelea katika gereza la Industrial Area na kumpima na kupata hali yake ya kiafya imeendelea kudorora.

Kiongozi wa mashtaka Sonnia Njoki na wakili Suleiman Bashir walieleza mahakama “afya ya mtu hupewa kipaumbele na kamwe hawapingi mshtakiwa kupelekwa Nairobi Hospital.”

Hakimu aliamuru mshtakiwa apelekwe hospitali chini ya ulinzi wa askari jela, watu wa familia yake wakiweka mikakati ya kumlipia dhamana hiyo ya Sh10 milioni na wadhamini wawili wa kiasi sawa na hicho.

Endapo mshtakiwa atashindwa kupata dhamana ya Sh10 milioni, mahakama ilimpa dhamana mbadala ya Sh5 milioni pesa taslimu.

Kesi hiyo itatajwa Machi 27, 2024, mshtakiwa aeleze ikiwa amekamilisha kulipa dhamana na pia kuripoti kama ametibiwa.

 

  • Tags

You can share this post!

Serikali yasitisha zabuni za mashirika ya umma kukata...

Maafisa wachunguza vifo vya watu wawili Makadara

T L