Habari za Kitaifa

Chopa iliyombeba Murkomen ina historia ya hitilafu ikipaa

March 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

IMEBAINIKA kuwa ndege iliyoanguka mnamo Jumamosi ilipokuwa ikipaa ikiwa imembeba Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen na mwenyekiti wa Mamlaka ya Kusimamia Viwanja vya Ndege (KAA) Caleb Kositany, imehusika kwenye visa kadhaa vya hitilafu za kimitambo.

Kisa hicho kilifanyika katika eneo la Mwachon, Eldama Ravine, Kaunti ya Baringo, Jumamosi asubuhi.

Kulingana na polisi, hakuna maafa yaliyotokea, ijapokuwa hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa kuhusiana na kisa hicho.

Huku taasisi husika zikiendelea kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio hilo, uchunguzi wa kina umebaini kwamba chopa hiyo aina ya Bell 407, nambari ya usajili 5Y-PKI, imehusika katika visa viwili kama hiyo kwa muda wa miaka sita iliyopita.

Ndege hiyo ni ya kibinafsi, na imekuwa ikifanyiwa ukarabati wa kimitambo na kuruhusiwa kuendelea kuhudumu kila  baada ya tukio.
Mnamo Agosti 2020, ndege hiyo ilishindwa kupaa baada ya kukumbwa na matatizo ya kimitambo katika Kaunti ya Kericho, ilikokuwa imepangiwa kuwarejesha aliyekuwa Waziri wa Afya Mutahi Kagwe na Mkurugenzi wa Matibabu Patrick Amoth jijini Nairobi.

Kutokana na tukio hilo, Waziri na ujumbe wake walilazimika kutumia magari kurejea jijini.

Mnamo Aprili 14, 2018, chopa hiyo iliharibika kidogo, baada ya mkia wake kugonga waya kwenye ua uliouzunguka Uwanja Mdogo wa Kakamega.

Kulingana na ripoti ya Kitengo cha Uchunguzi wa Ajali za Ndege katika Wizara ya Uchukuzi (AAID), ndege hiyo iliharibika wakati rubani wake alikuwa akijaribu kuiegesha.

“Mamlaka ya Uchukuzi wa Ndege (KCAA) inafaa kushirikiana na taasisi zifaazo za Kudumisha Viwanja vya Ndege kuhakikisha vina miundo sawa ili kuzuia matukio mengine ya mkia wa ndege kuharibiwa,” ikasema KCAA kwenye ripoti hiyo.

Kisa hicho kinajiri baada ya watu wawil kufariki Jumanne wiki hii, baada ya ndege mbili kugongana angani katika Uwanja wa Ndege wa Wilson, Nairobi.