Habari za Kitaifa

Chuo chabadilisha miraa kuwa chai na dawa

Na ELVIS ONDIEKI October 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

CHUO Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Meru kimewasilisha ombi la kupata hati miliki ya sacheti maalum ya miraa, kikitarajia kubadilisha kabisa jinsi watu wanavyotumia mmea huo maarufu kutoka eneo la Meru.

Badala ya kutafuna miraa kwa muda mrefu, watumiaji sasa wataweza kuitengenezea kama chai kwa kutumia sacheti hiyo inayofanana na ya majani ya chai, hatua inayochukuliwa kama mabadiliko ya kiteknolojia katika matumizi ya miraa.

Kulingana na maombi yaliyowasilishwa kwa Taasisi ya Kitaifa ya Mali Miliki (KIPI), sacheti hiyo itawezesha watumiaji kutumia miraa kama kichangamshi bila madhara makubwa ya kiafya.

“Bidhaa hii ya kutengeneza mchanganyiko unaoyeyuka kwa urahisi hutoa kichangamshi kwa athari ndogo. Hii inabadilisha utaratibu wa kawaida wa kutafuna miraa,” inasema sehemu ya maombi hayo.

Sacheti hiyo inaweza kutumiwa kwa kuwekwa kwenye maji ya kunywa,juisi, chai, chakula na dawa.

Mvumbuzi wa teknolojia hii ni Prof Joshua Mbaabu Arimi, mtaalamu wa sayansi ya chakula ambaye ana shahada ya uzamili katika uhandisi wa uhifadhi wa chakula kutoka Chuo Kikuu cha Katholieke Leuven (Ubelgiji) na uzamifu kutoka University College Dublin (Ireland).

Katika maelezo yake, chuo kinasema kuna mbinu maalum ya kukausha miraa inayotumika ili kudumisha ubora na uwezo wake wa kuchangamsha.

Pia, wameongeza ladha na viambato vya kuboresha utamu na uthabiti wa mchanganyiko huo.

Bidhaa hiyo ya sacheti inadaiwa kuwa na uwezo wa kusaidia kupunguza matatizo kama msongo wa mawazo, uchovu, unene uliozidi, vidonda vya tumbo, kukosa usingizi na njaa ya mara kwa mara.

Ingawa chuo hicho ndicho cha kwanza kuomba hati miliki, wafanyabiashara binafsi tayari wanauza sacheti za miraa mitandaoni.

Marqan Herbal huuza kwa Sh377 kwa sacheti moja nayo Handasjuice.com huuza bidhaa inayoitwa Jaba tea bags kwa Sh500 kwa sachet.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA) sekta ya miraa huingizia Kenya zaidi ya Sh13 bilioni kila mwaka.

Asilimia 80 ya miraa huzalishwa na kuliwa nchini, huku asilimia 20 ikisafirishwa nje, hasa Somalia.

Miraa ya Meru imegawanywa kwa aina tano: Kangeta, Kisa Gredi 1, Kisa Gredi 2 (Nyeusi), Kata, na Alele.

Kwa upande wa Embu, aina zote nne za miraa hujulikana kama muguka, nazo ni: mchele, medium, digital, na CR.

Uvumbuzi huu unajiri wakati serikali imeorodhesha miraa kama zao la kitaifa tangu mwaka 2016, hatua iliyotoa sera za kukuza, kudhibiti na kulinda biashara ya zao hili lenye utata.

Ikiwa hati miliki itatolewa, sacheti ya miraa huenda ikabadilisha kabisa namna inavyotumiwa, na kufungua milango mipya ya soko la kimataifa kwa wakulima wa miraa nchini Kenya.