Chuo Kikuu cha Nairobi chamfuta Prof Kiama baada ya kuvurugana kwa muda
BARAZA la Chuo Kikuu cha Nairobi limetangaza kuwa Naibu Chansela aliyesimamishwa kazi Prof Stephen Kiama, sasa amepigwa kalamu baada ya mizozo ambayo imekumba taasisi hiyo kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Katika barua iliyoandikwa Oktoba 14, 2024, mwenyekiti wa baraza hilo Prof Amukowa Anangwe alisema baraza hilo limetamatisha huduma za Prof Stephen Kiama.
Kulingana na baraza hilo, Prof Kiama alikoma kuwa naibu chansela mnamo Septemba 27.
“Baraza lingependa kufahamisha jamii ya Chuo Kikuu kwamba huduma za Prof Stephen Gitahi Kiama kama mfanyakazi wa Chuo Kikuu cha Nairobi zilitamatishwa kuanzia Septemba 27, 2024,” barua hiyo ilisema.
Prof Kiama na baraza hilo walikuwa wakigongana na kutimuliwa kwake sasa kunaweka bayana hatima yake. Mkataba wake ulipaswa kumalizika Januari 2025.
“Jamii ya chuo inapaswa kuwa na uhakika kwamba wakati wowote, baraza litasimama na kutekeleza majukumu yake kwa uaminifu na kwa kuzingatia sheria,” mwenyekiti wa baraza hilo Prof Amukowa Anangwe alisema.
Mnamo Agosti 3, Baraza kuu la Chuo Kikuu cha Nairobi lilimsimamisha kazi Prof Kiama kwa muda wa miezi mitatu, jambo lililozua mzozo mwingine kati yake na wakuu wa chuo hicho.
Baraza hilo lilimwagiza Margaret Jesang Hutchinson kuchukua nafasi ya Naibu Chansela.
“Katika kikao cha Baraza la Chuo Kikuu kilichofanyika Ijumaa, Agosti 2, 2024, tuliazimia kumsimamisha kazi Naibu Chansela, Profesa Stephen Kiama kwa muda wa miezi mitatu, ili kupisha uchunguzi unaoendelea kuhusu mwenendo wake, zikiwemo tuhuma za utovu wa nidhamu na ukaidi. Baraza hilo pia liliamua kuchukua hatua za kinidhamu kwa masuala ya ukaidi na utovu wa nidhamu uliokithiri. Wakati wa kusimamishwa kazi kwa Profesa Kiama, wafanyakazi na wanafunzi wote wanaagizwa kutojihusisha naye katika masuala rasmi ya chuo kikuu,” akasema Prof Anangwe wakati huo.
Masuala ya utawala yamekumba taasisi hiyo ya elimu ya juu na kuonekana kuchukua mkondo wa kisiasa baada ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kujiingiza katika mzozo uliomkabili Prof Kiama na baraza la chuo kikuu.
Kiini cha tofauti hizo ni vita vya urithi kwani kandarasi ya Profesa Kiama inafikia kikomo Januari 5, 2025. Ingawa Prof Kiama aliomba kuongezewa muda, vyanzo vilisema kuwa baraza hilo halikuwa na nia kufanya hivyo.