CIPK yataka mahakama ya rufaa ya kadhi kusikiza kesi za urithi
NA TITUS OMINDE
BARAZA la Wahubiri na Maimam (CIPK) linataka bunge kubuni sheria ya kuanzishwa kwa mahakama ya rufaa ya Kadhi kushughulikia masuala yanayofungamana na sheria za urithi na maswala mengine yanayofungamana na mali kwa kuzingatia muongozo wa qurani.
Wakihutubu wakati wa kufunguliwa kwa msikiti wa Masjid Al-Huda Centre mjini Eldoret eneobunge la Soy, Kaunti ya Uasin Gishu walisema ukosefu wa mahakama ya rufaa ya kadhi umefanya waislamu kutegemea korti za kawaida ambazo hutoa uamuzi kinyume na imani hiyo.
Wakitoa mfano wa kesi moja ya hivi maajuzi ambapo mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa alipata afueni ya kurithi mali ya baba mzazi baada ya korti ya kadhi kutupilia mbali kesi hiyo.
Sheikh Abubakari Bini alisema ni kinyume na imani ya dini hiyo kwa mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa kupata urithi wa baba mzazi.
“Juzi tulishangazwa na uamuzi wa mahakama wa kuruhusu mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa kupokea urithi hasa baada ya mahakama ya kadhi kutupilia mbali kesi yake. Kesi kama hizo zimetufanya kutaka kupewa korti ya kadhi ya rufaa kushughulikiwa rufaa za aina hiyo badala ya kutumia korti za kawaida,” alisema Sheikh Bini.
Msimamo wa Sheikh Bini uliungwa mkono na mzee wa dini hiyo, Ali Albeity ambaye alisema kwa muujibu wa imani yao mtoto kama huyo anapaswa tu kupewa zawadi na wala si urithi.
“Uamuzi wa mahakama ya rufaa kumpa mtoto kama huyo haki ya urithi ni hatari kwetu kwani sheria ya imani yetu inapinga mtoto kama huyo kupata urithi,” alisema Bw Albeity.
Kwa sasa viongozi hao wameanzisha mchakato wa kuasilisha hoja yao bungeni ili kubuniwa kwa mahakama ya kadhi ya rufaa.