Habari za Kitaifa

CITAM pia, yakataa siasa kwao

Na CHARLES WASONGA June 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KANISA la Christ Is The Answer Ministries (CITAM) limesema linakubaliana na wito wa vijana wa Gen-Z kutowaruhusu wanasiasa kuongea katika makanisa yake kote nchini.

Kwenye taarifa aliyoitoa Jumamosi Juni 29, 2024, Askofu Msimamizi wa Kanisa hilo Calisto Odede alisema miito ya vijana hao, walioandamana kupinga Mswada wa Fedha 2024, imezindua Kanisa kupiga marufuku makanisa yao kuingizwa kisiasa au kutumika na wanasiasa kuendeleza ajenda zao.

“Ama kwa kweli wametuonyesha kwamba kama viongozi wa kanisa, hatufai kuingiza siasa katika Ukristo na pia hatufai kuingiza Ukristo katika siasa,” akasema Askofu Odede.

Tangu wiki jana, vijana wa Gen-Z wamekuwa wakiendesha kampeni kali ya kuonya uongozi wa makanisa mbalimbali nchini kukoma kutoa nafasi kwa wanasiasa kuhutubu kwenye madhabahu yao.

Mnamo Jumapili, Juni 23, 2024, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kianglikana Nchini (ACK) Jackson Ole Sapit aliitikia wito wa vijana hao alipotupilia mbali ombi la Naibu Rais Rigathi Gachagua kwamba mbunge moja ahutubie waumini katika Kanisa la ACK Nyahururu.

Ilikuwa ni wakati wa ibada maalum ya kumtawaza Samson Mburu Gathathi kuwa Askofu mpya wa kanisa hilo, ambayo pia ilihudhuriwa na Rais William Ruto.

Askofu Calisto pia aliwasifu vijana wa Gen-Z kwa kufanya maandamano ya amani kote nchini kupinga mswada huo uliopendekeza kuwaongezea Wakenya mzigo wa ushuru.

“Inafurahisha kwamba maandamano yao hayakushawishiwa na siasa au semi za kikabila,” akaeleza.

Askofu Odede, hata hivyo, alisikitika kuwa maafisa wa polisi waliwakabili waandamanaji hao kwa nguvu kupita kiasi na kusababisha maafa.

“Tunapendekeza kwamba uchunguzi kamili ufanywe kuhusu hatua ya polisi kuwashambulia waandamanaji ambao hawakuwa na silaha zozote. Wahusika wote waadhibiwe kwa mujibu wa sheria,” akasema.

Askofu huyo alitoa rambirambi zake na kanisa la CITAM kwa familia za vijana waliopoteza maisha katika makabiliano hayo.

“Aidha, tunawatakia afueni ya haraka wale waliojeruhiwa na wamelazwa katika hospitali mbali mbali nchini,” Askofu Calisto akaongeza.

Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu (KNHRC) Ijumaa wiki jana ilithibitisha kuwa watu 23 waliuawa katika maandamano ya Jumanne, Juni 25, 2024 huku 53 wakipokea matibabu baada ya kujeruhiwa.

Aidha, tume huyo ilisema watu 345 walikamatwa katika purukushani hizo.