• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
CJ Koome akaa ngumu kuhusu kilio cha Wakili Ahmednassir 

CJ Koome akaa ngumu kuhusu kilio cha Wakili Ahmednassir 

NA RICHARD MUNGUTI

JAJI Mkuu (CJ) Martha Koome na majaji wengine sita wa Mahakama ya Juu wameomba Mahakama Kuu ifutilie mbali kesi ya wakili tata Ahmednassir Abdullahi ya kupinga marufuku asiwasilishe kesi mbele yao.

Jaji Koome, Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu, Majaji Mohammed Ibrahim, Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u, Isaac Lenaola na William Ouko walimweleza Jaji Enock Chacha Mwita kwamba “kisheria Mahakama Kuu haiwezi kuhoji maamuzi ya Mahakama ya Juu.”

Kupitia mawakili Ochieng Oduol na Kamau Karori  majaji hao saba walioshtakiwa na Chama cha Mawakili Nchini (LSK) walisema uamuzi wao wa kumzuia Bw Abdullahi ama kampuni yake ya mawakili kuwasilisha kesi mbele yao “hauwezi kubatilishwa na Mahakama Kuu.”

Katika mawasilisho yao Ijumaa mbele ya Jaji Mwita, Mabw Oduol na Karori walisema “maamuzi ya Mahakama ya Juu ndio utatoa mwelekeo kwa Mahakama nyingine zote nchini na kwamba Mahakama kuu haina mamlaka kisheria kuhoji uamuzi wowote wa Mahakama ya Juu.”

Mawakili hao wanaowakilisha Majaji hao saba walimweleza Jaji Mwita hana budi ila kutupilia mbali kesi hiyo ya LSK.

Mnamo Januari 2024 Msajili wa Mahakama ya Juu Bi L M Wachira alimwandikia barua Bw Abdullahi na kumweleza aidha yeye au wakili yeyote kutoka afisi yake hawapaswi kuwasilisha kesi yoyote katika Mahakama ya Juu kutokana na kile walichosema ni matamshi yake ya dharau kuwahusu kwa miaka kadhaa sasa.

Kutokana na mwenendo huo wake mahakama hiyo ilimpiga marufuku kuwasilisha kesi mbele yake.

Lakini mawakili Issa Mansur na Wilfred Nderitu walitofautiana na mawakili Oduol na Karori wakisema Mahakama Kuu ina mamlaka kuhoji maamuzi ya Mahakama ya Juu.

Bw Mansur alisema uhuru na kinga ya kisheria dhidi ya majaji wa Mahakama ya Juu unaweza kuhojiwa na Mahakama Kuu aliyosema ina mamlaka asili.

Bw Mansur alisema majaji hao saba hawapaswi kutumia kama ngao sheria kuvuruga haki za Bw Abdullahi na kampuni yake ya mawakili.

Wakili huyo aliomba Jaji Mwita atupilie mbali ombi la majaji hao saba na kuagiza kesi waliyoshtakiwa na LSK isikizwe na kuamuliwa.

Jaji Mwita atatoa uamuzi ikiwa kesi ya LSK ya kubatilisha marufuku hayo dhidi ya Abdullahi ina mashiko kisheria au la mnamo Juni 21, 2024.

  • Tags

You can share this post!

Mtangazaji Weldon Kirui asikitika redio zimesheheni...

Athari za vita vya Israel-Iran kwa Kenya

T L