Cop Shakur na wenzake waachiliwa kwa dhamana na masharti makali
Wanaume watatu wanaodaiwa kuwa wanachama wa kundi linalojulikana kama ‘Kenyan FBI’ Patrick Osoi, Jackson Kihara almaarufu Cop Shakur, na Hiram Kimathi, jana waliachiliwa kwa dhamana na Mahakama ya Kahawa, baada ya kushtakiwa kwa kuhusika katika shughuli za uhalifu.
Hakimu Richard Koech aliachilia kila mmoja dhamana ya Sh 200,000, au Sh50 pesa taslimu. Hata hivyo, kuachiliwa kwao kulitolewa kwa masharti kali ili kuhakikisha kuwa uchunguzi unaoendelea haujatatizwa.
Upande wa mashtaka ulikuwa umeomba washukiwa wazuiliwe kwa muda zaidi, kwa madai kuwa walikuwa tishio kwa usalama wa taifa. Serikali ilisema uchunguzi bado unaendelea na walihitaji muda wa kutosha kufanya upekuzi katika makazi ya washukiwa.
“Washukiwa wanaweza kuingilia uchunguzi iwapo wataachiliwa kwa sasa,” upande wa mashtaka uliambia mahakama.
Licha ya hoja hiyo, mahakama iliruhusu washukiwa kuachiliwa kwa dhamana lakini kwa masharti wasijihusishe na uhalifu mwingine wowote wakati wa kipindi cha dhamana, wasiingilie au kuwatisha mashahidi na wasitatize haki kwa njia yoyote
Vile vile, waliagizwa wafike kwa maafisa wa uchunguzi mara moja kwa wiki na wafike mahakamani kila mara wakihitajika
Masharti haya yanalenga kuhakikisha kuwa washukiwa wanashirikiana kikamilifu na uchunguzi unaoendelea.