Habari za Kitaifa

Corona imerudi?

March 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

HELLEN SHIKANDA Na MERCY CHELANGAT

MADAKTARI wanatahadharisha kuwa kuna ongezeko la maambukizi ya magonjwa ya kupumua huku baadhi ya wataalamu wa afya wakiyahusisha na kurejea kwa Covid-19.

Data za kufuatilia maambukizi ya virusi vya SARS-Cov-2 (virusi vya corona) za sampuli zilizotolewa ukanda wa ziwa nchini zinaonyesha kuwa, Kenya inakumbwa na ongezeko la maambukizi ya aina ya corona ya Omicron, zinazoitwa JN.1 pamoja na virusi vya flu aina ya H1N1 ( wakati mwingine inaitwa homa ya nguruwe).

Aina ya virusi vya JN.1 imetajwa na Shirika la Afya Ulimwenguni kama inayotia hofu, na iliripotiwa mara ya kwanza Agosti 2023, nchini Iceland na Luxembourg.

Tangu wakati huo, tafiti kuhusu aina hii ya virusi zimeonyesha kwamba, ni tofauti na aina zinzine za Covid-19 na sana sana hugunduliwa miongoni mwa wasafiri na katika majitaka.

“Kuendelea kuongezeka kwa JN.1 kunaashiria kuwa, aina hiyo inasambaa haraka na ina uwezo mkubwa wa kuepa kinga ya mwili ikilinganishwa na aina zingine za virusi ambavyo tayari zinasambazwa,” ulieleza utafiti uliochapishwa katika jarida la Environmental Health mapema mwaka 2024.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa kutambua jinsi Covid-19 inavyosambazwa Dkt Shem Otoi, ongezeko la sasa la maambukizi sio la kushangaza kwa sababu limewahi kuwepo.

“Tunapochunguza data zilizopita, kinachofanyika sasa kinaweza kutambua kipindi hiki kama kilele cha Covid-19, isipokuwa hii inaweza kuwa sio mbaya sana,” alisema.

Dkt Otoi anasema kwa muda, wamegundua kwamba, aina nyingi za virusi zilizoisha makali kama Omicron, Alpha na Delta, huwa nafasi yake inachukuliwa na aina inayofanana au aina mpya kabisa baada ya kila miezi sita.

Kulingana na Dkt Ahmed Kalebi, ambaye ni mwanapatholojia huru, kumekuwa na ongezeko la magonjwa ya mfumo wa kupumua nchini katika kipindi cha wiki mbili zilizopita na watu wengi wana dalili za flu kama kikohozi, uchungu kooni, maumivu ya kifua na kutokwa makamasi puani.

“Hizi ni dalili za maambukizi ya mfumo wa kupumua. Hata hivyo, sio hali ngeni au isiyotarajiwa kwa kuwa ni msimu wa flu,” akasema Dkt Kalebi.

“Katika msimu wa Flu huwa kuna ongezeko la maambukizi ya maradhi ya virusi ikiwemo mafua, corona na mengine. Kama unakumbuka, Covid-19 iliongezeka sana msimu sawa na huu,” alisema

Alieleza ingawa Wizara ya Afya haipimi au kufuatilia kwa kiwango kikubwa, kuna uwezekano baadhi ya Wakenya wanajipima wakiwa nyumbani kwa kutumia vifaa vya kujipima.

Hata hivyo alisema idadi kamili ya maambukizi huenda isijulikane.

“Hii inafanya iwe vigumu kujua hali halisi nchini,” alieleza.

“Huenda hatutawahi kujua kikamilifu iwapo kuna ongezeko la visa vya maambukizi ya Covid-19 kwa kuwa hakuna ufuatiliaji unaofanywa. Katika nchi kama Amerika, wanaweza kufuatilia kupitia kupima majitaka na kushauri watu kukiwa na ongezeko la maambukizi,” alisema.

Dkt Kalebi alisema kwamba, ukweli kwamba sasa watu wako na kinga dhidi ya maambukizi ya awali ya Covid-19 kutokana na chanjo, ugonjwa huo hautakuwa na makali yanayoweza kusababisha kifo.

Hata hivyo anasema Covid-19, kama maradhi mengine ya mfumo wa kupumua inaweza kusababisha magonjwa yanayoweza kufanya mtu kulazwa hospitalini na hata kufariki kama walio na kinga hafifu ya mwili kama vile watoto wadogo na wazee.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Matibabu Dkt Sultani Matendechero, aliambia Taifa Leo kwamba, data za ufuatiliaji nchini zinaonyesha kuwa kiwango cha maambukizi kinaendelea kupungua lakini akashauri umma kupata chanjo nyingi za kuimarisha kinga iwezekanavyo.

“Bado tuko na chanjo ya Covid-19 na watu wanapaswa kuzitumia. Covid- 19 ingali inasambazwa,” alisema.