Dakika za mwisho za Jirongo kabla afariki
WATU kadhaa wameelezea dakika za mwisho za aliyekuwa Mbunge wa Lugari, Cyrus Jirongo, kabla ya kufariki katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea alfajiri ya Jumamosi katika eneo la Karai, Kaunti ya Naivasha, kwenye Barabara Kuu ya Nairobi–Nakuru.
Dakika kumi na tano baada ya saa nane usiku, Bw Jirongo, aliyekuwa akiendesha gari lake mwenyewe aina ya Mercedes-Benz rangi nyeupe akiwa peke yake ndani, aliingia katika Kituo cha Mafuta cha Eagol kilichoko Karai. Alikuwa akielekea Nairobi, na kituo hicho kiko upande wa pili wa barabara.
Walioshuhudia walisema alipofika katika kituo hicho, alionekana kama alitaka kuelekea kwenye pampu ya kujaza mafuta.
Hata hivyo, alipita pampu zote, akageuza gari na kurejea barabarani. Alipokuwa akijiunga tena na barabara kuu ndipo kosa hatari lilipotokea.
Kwa mujibu wa maelezo ya mhudumu wa kituo cha mafuta aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, Bw Jirongo aliingia barabarani lakini akaendelea kuendesha gari katika laini inayotumiwa na magari yanayotoka Nairobi kuelekea Nakuru, yaani njia ya magari yanayotoka upande aliokuwa akielekea.
“Nilisikia kishindo kikubwa sana,” alisema mhudumu huyo.
Mercedes-Benz aliyokuwa akiendesha Bw Jirongo iligongana na basi la kampuni ya Climax lililokuwa likisafiri kutoka Nairobi kuelekea Nakuru.
Baada ya mgongano huo mkali, gari la Bw Jirongo liliburutwa umbali wa mita chache kutoka eneo la ajali kabla ya basi hilo kusimama kabisa.
Mhudumu huyo alisema alikimbia eneo la ajali na kujaribu kufungua mlango wa gari, lakini ulikuwa umefungwa.
“Niliangalia ndani nikamwona mtu ameinamia usukani, uso ukiwa umeelekea chini, na kulikuwa na damu kichwani,” alisema.
Alisema alipiga simu ya dharura saa nane na dakika 37 usiku kuwaarifu polisi kabla ya kujaribu kusimamisha lori kuomba usaidizi.
Hata hivyo, dereva wa kwanza hakusimama.
Dakika chache baadaye, dereva mwingine alisimama na wakaanza juhudi za kumsaidia dereva wa Mercedes-Benz, lakini waligundua kuwa tayari alikuwa amefariki.
Dereva wa basi la Climax, Bw Tirus Kamau, alithibitisha simulizi hilo lakini akaongeza kuwa kulikuwa na msongamano mdogo wa magari katika laini yake kabla ya ajali.
Alisema Bw Jirongo alijaribu kupita gari jingine na akaingia kwenye laini yake, hali iliyosababisha mgongano huo.
Bw Kamau, ambaye ana uzoefu wa zaidi ya miaka minane barabarani, alisema alikuwa amebeba abiria 65, huku Bw Jirongo akiwa peke yake.
“Nilikuwa nikielekea Busia kutoka Nairobi. Gari la Mercedes-Benz lilikuwa linakuja kutoka upande wa pili. Alijaribu kupita, ndipo tukagongana,” alisema.
Ripoti ya polisi ilieleza kuwa Bw Jirongo, mwenye umri wa miaka 64, alikuwa akiendesha gari lenye nambari ya usajili KCZ 305C kutoka Nakuru kuelekea Nairobi aliposhindwa kudumisha njia yake na kugongana na basi lenye nambari KCU 576A.
Alipata majeraha makubwa ya kichwa na kufariki papo hapo.
Kamanda wa Trafiki wa Kanda ya Bonde la Ufa, Bi Sara Chumo, alithibitisha maelezo ya ajali hiyo.
Mwili wa marehemu ulipelekwa katika mochari ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Naivasha kabla ya kuhamishiwa katika mochari ya Lee, jijini Nairobi.
Magari yaliyohusika yalikokotwa hadi Kituo cha Polisi cha Naivasha, yanakozuiliwa kwa uchunguzi zaidi. Polisi walisema wanashuku huenda marehemu alikuwa na silaha wakati wa ajali, ingawa haikupatikana.
Bw Jirongo alikuwa maarufu kwa kuongoza vuguvugu tata la Youth for Kanu ’92 (YK92) lililounga mkono kampeni ya kuchaguliwa tena kwa Rais Daniel arap Moi mnamo 1992.
Alihudumu kama Mbunge wa Lugari kwa mihula miwili na baadaye alihusishwa na vyama kadhaa vya kisiasa. Pia, aliwahi kuwa Waziri wa Maendeleo ya Maeneo ya Mashambani na aliwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2017.