Habari za Kitaifa

Daktari atupwa jela miaka 12 kwa kupanga shambulio kwa kutumia bakteria ya kimeta

April 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA RICHARD MUNGUTI

DAKTARI amehukumiwa kifungo cha miaka 12 jela, kwa kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi.

Dkt Mohamed Abdu Ali, aliyekuwa akihudumu katika Hospitali ya Makueni Level Four, alihukumiwa na Hakimu Mkuu Martha Mutuku.

Kifungo hicho kinaaanza Aprili 29, 2016, alikozuiliwa na polisi. Alihukumiwa kwa kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi la Islamic State (ISIS).

Dkt Mohamed Ali aliyehukumiwa miaka 12 jela kwa kushiriki ugaidi na kuwa mwanachama wa kundi la ISIS. Picha|Richard Munguti

Mahakama ilimpata na hatia ya kupanga shambulio la kigaidi kwa kutumia bakteria hatari ya maradhi ya kimeta.

Kulingana na mpango wa Dkt Ali na washirika wake walio nje ya nchi, lengo lao lilikuwa kuweka viini hatari katika seli za mwanadamu, hivyo kusababisha kifo cha ghafla kwa waathiriwa.

Kwenye hukumu iliyotolewa na Bi Mutuku, Dkt Ali alipatikana na hatia kwa makosa matano ya kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi, kupanga mkutano wa kuunga mkono na kuendeleza shughuli za kundi la kigaidi, kuwaingiza watu katika ugaidi, kukusanya habari akiwa na lengo la kutekeleza shambulio la kigaidi na kumiliki maandishi yanayohusiana na utekelezaji wa kitendo cha kigaidi.

Hata hivyo, mahakama ilimwondolea kosa mkewe mshtakiwa, Bi Nuseiba Mohamed Haji Osman au Umm Fidda, aliyekuwa ameshtakiwa pamoja na mumewe katika mashtaka hayo yote.

Mahakama ilisema kwamba hakukuwa na ushahidi wowote wa kumhusisha na makosa hayo.