Habari za Kitaifa

Dawa ya kulevya ya Sh8.2 bilioni yakamatwa baharini Mombasa

Na  ANTHONY KITIMO October 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Jeshi la Wanamaji la Kenya (Kenya Navy) kwa ushirikiano na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) chini ya Mkurugenzi Mohamed Amin, limefichua jinsi maafisa wa usalama wa Kenya walivyofanikiwa kukamata meli na kupata zaidi ya kilo 1,000 za dawa za kulevya aina ya methamphetamine ya thamani ya zaidi ya Sh8.2 bilioni.

Kukamatwa kwa dawa hizo kulitokana na operesheni ya mashirika mbalimbali ya usalama ikiwemo Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Jeshi la Wanamaji la Kenya, Walinzi wa Pwani (Kenya Coast Guard), Polisi wa Bandari, Huduma ya Ujasusi wa Kitaifa (NIS), Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA) na Polisi wa Mamlaka ya Bandari (KPA Police).

“Vita dhidi ya usafirishaji wa dawa za kulevya ni jitihada ya kimataifa. Tunashukuru Jeshi la Wanamaji na maafisa wengine wa kimataifa kwa kusaidia kukomesha biashara hii hatari. Ushirikiano wa kikanda umewezesha kukamatwa kwa chombo hiki kilichokuwa kikiendesha shughuli  hatari katika Bahari ya Hindi Magharibi,” alisema Bw Amin.

Meli hiyo isiyosajiliwa, ikiwa na wafanyakazi sita wenye asili ya Kiajemi (Iran), ilinaswa na timu ya kimataifa ya mashirika mbalimbali takribani kilomita 630 mashariki mwa Mombasa na kisha kupelekwa hadi Bandari ya Mombasa chini ya ulinzi mkali.

Naibu Kamanda wa Jeshi la Wanamaji, Brigedia Sankale Kiswaa, alisema kuwa meli hiyo ilikuwa ikifuatiliwa chini ya kampeni ya Bahari Safi, lakini ikakamatwa kabla haijafika ufukweni.

“Katika oparesheni hii tuliyoshirikiana na mashirika ya kimataifa ya polisi, tuliweza kukamata meli hiyo ikiwa na raia sita wa Iran. Tulipopekua sehemu ya chini ya meli, tulipata kilo 1,024 za methamphetamine, dawa ya  kulevya yenye thamani ya zaidi ya Sh8.2 bilioni,” alisema Brigedia Kiswaa.

Bw Amin alisema kuwa meli hiyo ilikuwa na vifurushi 769.

“Tunaendelea kuwahoji washukiwa hao sita, ingawa bado hatujabaini ilikotoka shehena hii. Tumehifadhi ushahidi wa awali unaoonyesha kuwa dawa hizo zilikuwa zikielekezwa kwenye soko la ndani nchini Kenya,” aliongeza Bw Amin.

Alisema washukiwa hao watafikishwa mahakamani Jumatatu, baada ya taratibu za uchunguzi kukamilika.

Kulingana na ripoti ya Mwanakemia wa Serikali sampuli zilizochukuliwa zilionyesha kuwa dawa hiyo ni methamphetamine safi kwa asilimia 98.

Mkurugenzi wa Kenya Coast Guard, Bruno Shioso, pia alihudhuria kikao cha kutoa taarifa kwa wanahabari kuhusu tukio hilo.

Dawa hii huonekana kama unga au vidonge vinavyofanana na vipande vya kioo.

Hutumiwa kwa njia mbalimbali: kumezwa, kunuswa, kuvutwa kama moshi au kudungwa sindano.

Kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), methamphetamine huchochea hali ya furaha ya ghafla na kuongeza nguvu ya kimwili na kiakili, huku watumiaji wakihisi wana uwezo wa kufanya kazi nyingi bila uchovu au njaa.

Watumiaji wa dawa hii hupata ongezeko la kasi ya mapigo ya moyo, shinikizo la damu, na joto la mwili, jambo linalosababisha jasho na wasiwasi.

Kwa dozi kubwa, huweza kusababisha mshtuko wa moyo, kiharusi, au kifo kutokana na kushindwa kupumua.

Matumizi ya muda mrefu ya methamphetamine husababisha utapiamlo, kupungua kwa uzito, na  kuitegemea. Wale wanaoacha kuitumia ghafla hukumbwa na usingizi wa muda mrefu na msongo wa mawazo.