Habari za Kitaifa

Dawa za kulevya zilizotoweka zilifichwa kambi ya jeshi, maelezo mapya yaibuka

Na BRIAN OCHARO January 8th, 2026 Kusoma ni dakika: 3

WANAJESHI wanane wameshtakiwa rasmi kwa ulanguzi wa dawa za kulevya huku maelezo mapya yakiibuka kwamba sehemu ya mihadarati hiyo ilifichwa katika kambi ya jeshi.

Hayo yalijiri huku thamani ya mihadarati iliyoporwa kutoka kwa meli iliyokamatwa katika Bahari ya Hindi mnamo Oktoba mwaka uliopita ikiongezeka hadi zaidi ya Sh330 milioni kutoka Sh192 milioni.

Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma na Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya zilieleza Mahakama ya Hakimu ya Mombasa kuwa, gramu 38,756 za dawa aina ya methamphetamine ziliporwa kutoka kwenye mzigo mkubwa wa kilo 1,024 uliokadiriwa kuwa na thamani ya Sh8.2 bilioni wakati wa operesheni iliyoendeshwa Oktoba 19.

Wanajeshi hao pamoja na raia wengine wawili walifikishwa mahakamani Jumanne.

Juma Mwinyifaki anakabiliwa na mashtaka ya ulanguzi wa gramu 2,601 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh20.8 milioni, ambazo alidaiwa kuhifadhi kichakani katika Kambi ya Jeshi ya Mtongwe, Likoni, Novemba 27.

Peter Kipng’etich Tonui na Mustafa Salim Johari wanakabiliwa na mashtaka ya kupanga njama ya kufanya ulanguzi wa madawa ya kulevya.

Upande wa mashtaka unasema kuwa Novemba 25, katika eneo la Majengo Mapya, Mvita, wawili hao walipanga kuhusika katika ulanguzi wa gramu 6,194 za dawa hizo zenye thamani ya Sh49.5 milioni, pamoja na mashtaka mengine ya ulanguzi.

Kundi jingine lililojumuisha Duke Nyamwaya, Dinah Moraa Obwocha na Elijah Mbogo linakabiliwa na mashtaka ya kupanga njama ya kufanya ulanguzi wa gramu 14,321 zenye thamani ya Sh114.6 milioni.

Nyamwaya na Mbogo pia wanadaiwa kuhusika katika ulanguzi wa gramu 5,380 zenye thamani ya Sh43 milioni, huku Nyamwaya na Moraa wakikabiliwa kando na mashtaka ya ulanguzi wa gramu 8,941 zenye thamani ya Sh71.5 milioni, ambazo zinadaiwa kuhifadhiwa katika nyumba.

James Ekiru na Abdirahman Abdi Kuno pia wameshtakiwa kwa kuhusika katika ulanguzi wa gramu 1,319 zenye thamani ya Sh10.5 milioni, pamoja na mashtaka ya kuhifadhi dawa hizo.

Michael Peter Kariuki na Abdulrehman Salad Jara wanakabiliwa na mashtaka sawa ya kuhusika katika ulanguzi wa gramu 2,535 za thamani ya takriban Sh20.2 milioni. Hata hivyo, washukiwa hao walikanusha mashtaka yote dhidi yao.

Wachunguzi wanasema mashtaka hayo yanatokana na njama ya ndani wakati wa operesheni, ambapo maafisa waliokuwa na jukumu la kulinda mzigo walidaiwa kuondoa sehemu ya madawa hayo kabla ya kuhifadhiwa rasmi kama vielelezo vya mahakama.

Washukiwa, kupitia kwa mawakili wao, waliomba mahakama iendelee na masharti ya dhamana ya Sh500,000, wakisema kuwa walihudhuria mahakama mara kwa mara bila kukosa, makazi yao yanajulikana, na waliheshimu masharti ya dhamana awali.

“Iwapo hawakutoroka wakati thamani ya madawa ilikuwa juu zaidi, sasa hakuna sababu ya kutoroka,” wakili alisema akiongeza kuwa washukiwa wanafamilia wanaowategemea.

Upande wa mashtaka ulipinga pendekezo hilo, ukisema kuwa hatari ya kutoroka na kuingilia ushahidi imeongezeka sasa baada ya washukiwa kufunguliwa mashtaka rasmi.

Upande wa mashtaka ulipendekeza dhamana iongezwe hadi Sh3 milioni, ikizingatiwa adhabu ya faini au kifungo cha hadi miaka 50 iwapo watapatikana na hatia. Mahakama itatoa uamuzi wake Januari 8.

“Kwa kuwa hatujui kesi hii itachukua muda gani, mahakama lazima ihakikishe kuwa watuhumiwa watahudhuria bila kukosa,” upande wa mashtaka ulisema, ukiongeza kuwa washukiwa hao hawako tena kwenye huduma ya KDF.

Mahakama pia imetoa agizo la kumtaka Bi Moraa ahudhurie mahakama baada ya kukosa kufika wakati wa kushtakiwa.

Wakili wake alieleza kuwa hakuwa na ufahamu wa kikao hicho na kwamba awali alikuwa ameondolewa katika orodha ya washukiwa.

“Aliletwa mahakamani Novemba 24 pamoja na wahusika wengine na aliachiliwa Desemba 8 baada ya DPP kuthibitisha kuwa hangeshtakiwa,” wakili alisema, akiongeza kuwa jina lake lilionekana kwenye karatasi ya mashtaka kutokana na makosa ya kiutawala au kisiasa.

Wanajeshi hao wanane walikuwa sehemu ya kikosi cha Jeshi la Wanamaji wa Kenya kilichotumwa kukamata meli aina ya MV Mashallah, iliyobeba kilo 1,024 za methamphetamine zilizokuwa zimetangazwa kimakosa kuwa ni kahawa.

Meli hiyo iliendeshwa na raia sita wa Iran ambao ni Jasem Darzaen Nia, Nadeem Jadgai, Imran Baloch, Hassan Baloch, Rahim Baksh na Imtiyaz Daryayi, ambao bado wanazuiliwa huku uchunguzi ukiendelea.