• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
DCI yaahidi kuvunja mitandao ya wizi wa magari

DCI yaahidi kuvunja mitandao ya wizi wa magari

NA WANDERI KAMAU

MKURUGENZI Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin, ameahidi kuongoza operesheni kali kunasa mtandao wa wahalifu ambao wanajihusisha na wizi wa magari.

DCI mnamo Jumamosi ilitangaza kwamba ilinasa magari zaidi ya wizi jijini Nakuru, huku maafisa wake wakimkamata mshukiwa mmoja wa wizi huo.

Hili linafuatia operesheni kama hizo, zilizoendeshwa katika kaunti za Nairobi na Nyeri.

Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin. PICHA | MAKTABA

Kwenye taarifa, idara hiyo ilisema kuwa maafisa wake waliwakamata washukiwa hao katika eneo la 58, viungani wa jiji la Nakuru, lakini mmoja wao akafanikiwa kutoroka.

“Katika eneo la 58, viungani mwa jiji la Nakuru, tuliwanasa washukiwa wawili; Michael Gichuhi Macharia na Charles Kung’u Kamau,” ikaeleza idara hiyo.

Mshukiwa wa kwanza, Michael Gichuhi, alipatikana na gari aina ya Toyota Vitz, lenye nambari za usajili KCW 582Q, linalodaiwa kuibwa kutoka kwa wakili mmoja jijini Nairobi.

Maafisa hao walimkamata mshukiwa wa pili, Charles Kamau, akiendesha gari ambalo halikuwa na nambari za usajili aina ya Toyota Probox.

“Baada ya uchunguzi, tulibaini kuwa gari hilo lina nambari za usajili KBV 958J. Hata hivyo, mshukiwa huyo alifanikiwa kutoroka baada ya mvutano wa muda na maafisa wetu. Tunaendelea na juhudi za kumtafuta,” ikaeleza idara hiyo.

Kwa miezi kadhaa iliyopita, kumekuwa na ongezeko kubwa la watu ambao wamekuwa wakilalamikia wizi wa magari katika makazi yao, hasa jijini Nairobi.

Kulingana na waathiriwa, wezi hao huwa wanatoa mitambo ya kubaini na kutambua mahali magari hayo yalipo ili kutokamatwa.

  • Tags

You can share this post!

Kuelimisha vijana tukipinga miradi ya kuwapa ajira ni kazi...

Safaricom kutoa simu za bei nafuu

T L