Dereva wa teksi aliyepinga ushuru wa barabara aondoa kesi
WAKENYA wameachwa kwa mataa baada ya mlalamishi aliyepinga hatua ya serikali ya kuongeza Ushuru wa kurekebisha Barabara kutoka Sh18 hadi Sh25 kwa lita kuondoa kesi hiyo.
Rekodi za mahakama zinaonyesha kuwa Bw George Odhiambo Juma, ambaye ni dereva wa teksi aliyewasilisha kesi hiyo, alirudi mahakamani na kuweka ombi lingine la kuiondoa kesi hiyo chini ya wiki moja baada ya kupata amri ya kuzuia serikali kuongeza ushuru huo.
Jaji Gregory Mutai alikubali ombi la Bw Juma la kuondoa kesi hiyo baada ya pande zote katika kesi hiyo kutowasilisha pingamizi yoyote.
“Washtakiwa hawajapinga kesi uondolewa. Katika hali hiyo, mahakama inaidhinisha kesi hiyo iondolewe na faili ya kesi ifungwe mara moja,” Jaji Mutai alisema katika agizo la Agosti 19.
Rekodi za mahakama zinaonyesha kuwa Bw Juma aliwasilisha notisi ya kuondoa kesi hiyo mnamo Agosti 16. Ombi hilo halikukabiliwa na upinzani wowote.
Siku tatu baadaye, mahakama ilikubali ombi hilo na kufunga faili.
Bw Juma aliwasilisha kesi hiyo mnamo Agosti 2, siku chache baada ya serikali kuongeza Kodi ya Kurekebisha Barabara kutoka Sh18 hadi Sh25 kwa lita.
Katika ombi lake, Bw Juma alilalamika kwamba serikali iliweka nyongeza hiyo mpya ya ushuru bila ushiriki wa kutosha wa umma.
Pia, alidai kuwa mkutano wa umma uliofanyika Julai 8 katika maeneo tofauti nchini kujadili pendekezo la nyongeza hiyo ulikosa ushiriki wa kweli.
“Vituo kumi vilivyotumika kufanya mkutano wa umma vilikuwa vichache mno. Hii ilizuia Wakenya wengi kufika katika maeneo hayo kutoa maoni yao kuhusiana na pendekezo la nyongeza ya ushuru wa kurekebisha barabara,” alisema.
Mlalamishi huyo aliendelea kudai kuwa utawala wa Rais William Ruto ulipanga siku moja pekee kwa zoezi hilo, ambalo halitoshi kufanya shughuli nzima ya kutoa maoni.
Alisema yeye mwenyewe hakuweza kushiriki kwa vile alikuwa akisafirisha abiria siku hiyo.
“Kama washtakiwa wangepanga siku zaidi za kukutana na umma kwa shuguli hii, ningekuwa na nafasi ya kutoa maoni yangu, na pia Wakenya wengi,” alieleza mahakama.
Mlalamishi huyo alidai kuwa Wakenya wengi kwa sasa wanakumbwa na matatizo ya kiuchumi, na kwamba kuongeza ada hiyo ni mzigo na wala si haki.
“Nyongeza ya ushuru kama inavyopendekezwa na serikali haina mashiko katika nyakati hizi ngumu za kiuchumi na haiendani na hali halisi. Wahusika wanafahamu haya lakini wameamua kupuuza,” alisema.
Mlalamishi aliambia mahakama kwamba aliyekuwa Waziri wa Barabara Kipchumba Murkomen (ambaye kwa sasa ni Waziri wa Michezo) alisema kuwa serikali itafanya uamuzi kulingana na mapendekezo ya umma, ambao walipinga kuongezwa kwa ushuru wa mafuta.
Kulingana na taarifa ya Wizara ya Barabara, nchi inakabiliwa na uhaba wa fedha ya kurekebisha barabara ya Sh78 bilioni mwaka huu wa fedha pekee.
Wizara hiyo iliongeza kuwa iwapo hali hiyo itaendelea, upungufu unatarajiwa kufikia Sh315 bilioni ifikapo mwaka wa fedha 2028/2029.
Hata hivyo, mlalamishi alidai kuwa serikali ilishindwa kuelimisha umma kuhusu ongezeko hilo, mantiki na athari zake.
“Wito wa kuwataka wananchi kuwasilisha maoni haukufaulu kama ilivyotarajiwa kwani wananchi wengi kwa kiasi kikubwa walibaki kutofahamu mchakato huo. Kwa mfano, mimi sikufahamishwa ni kwa nini kulikuwa na haja ya kuongeza ushuru huo,” alisema.
Mnamo Agosti 14, 2024, mahakama ilitoa amri za muda za kuzuia serikali kutekeleza sheria hiyo ya kuongeza ada ya kurekebisha barabara baada ya kuzingatia hoja za Bw Juma.
Hata hivyo, agizo hili la zuio la muda lilidumu kwa muda mfupi baada ya mlalamishi kuamua kuondoa kesi hiyo kabla ya kusikilizwa kikamilifu.