DJ Joe Mfalme kuzuiliwa siku 14 katika kesi ya mauaji ya polisi
NA RICHARD MUNGUTI
MCHEZA santuri Joseph Mwenda Munoru almaarufu DJ Joe Mfalme aliyekamatwa pamoja na watu wengine sita kwa kwa mauaji ya afisa wa polisi Inspekta Felix Kintosi, atasailia korokoroni kwa siku 14 ili makachero wakikamilisha uchunguzi.
DJ Mfalme alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Margaret Murage katika Mahakama ya Kibra, pamoja na Allan Ochieng, Simon Wambungu na Eric Gathua.
Mbali na DJ Mfalme maafisa watatu wa polisi Khadija Abdi Wako, Sammy Rotich na Agnes Mogoi pia walifikishwa kortini.
Maafisa hawa wa polisi watazuiliwa katika kituo cha polisi cha Riruta, huku mshukiwa mwingine Allan Ochieng akizuiliwa katika kituo cha polisi cha Kabete.
Washukiwa hao saba waliagizwa wazuiliwe siku 14 kuwezesha maafisa wa uchunguzi kukamilisha zoezi la kubaini kilichopelekea Inspekta Kintosi kuaga.
Ombi la kuwasukuma saba hao katika kituo cha polisi cha Muthangari liliwasilishwa na Inspekta Fredrick Kosen kutoka afisi ya uchunguzi wa jinai ya
Dangoreti DCI.
Aliomba washukiwa hao wazuiliwe kwa siku 21 lakini mahakama ikawapa polisi siku 14.
Lakini siku hizo zilipunguzwa kwa siku saba kufuatia ombi la mawakili wanaowawakilisha.
Washukiwa hao wanachunguzwa kwa mauaji ya Kintosi mnamo Machi 16, 2024 baada ya makabiliano karibu na kituo cha polisi cha Kikuyu.
Inadaiwa gari la DJ Mfalme liligonga gari la marehemu na wakati huo hakuna aliyejeruhiwa wakati wa kisa hicho.
Inasemakana kwamba maafisa hao wa polisi waliozuiliwa katika kituo cha Riruta walisaidia kumtia nguvuni marehemu katika kituo cha polisi cha Kikuyu.
“Marehemu alilalamika alikuwa na maumivu ya tumbo kisha akapelekwa hospitali na kulazwa,” Kachero Kosen alieleza mahakama.
Maafisa hao wa polisi wametiwa nguvuni kwa kutowajibika ipasavyo kwa vile kinachosemekana kwamba hawakumshughulikia mwenzao aliye lalamikia maumivu ya tumbo na kukojoa damu alipofikishwa katika kituo cha polisi cha Kikuyu.
Mahakama ilielezwa kuna mshukiwa mwingine ambaye hajatiwa nguvuni kuhusiana na majeraha ambayo Kintosi alipata.
Mahakama iliombwa muda polisi wachunguze kamera za CCTV ambapo marehemu alishambuliwa.
Bi Murage aliamuru washukiwa hao wasalie ndani hadi Aprili 8, 2024 atakapotoa maagizo zaidi.