Dorcas Rigathi aunga mpango wa wakfu kupambana na ulevi Kiambu
NA LAWRENCE ONGARO
KERO ya pombe na utumizi wa dawa za kulevya miongoni mwa vijana ni hatari na wanajamii wanafaa kuungana pamoja katika vita hivyo, amesema mke wa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Bi Dorcas Rigathi.
Bi Rigathi alisema ataungana pamoja na Naibu Gavana wa Kiambu Rose Kirika kuwazungumzia vijana kuhusu jinsi wanavyoweza kuepuka kero hiyo.
Alisema jamii imekuwa katika njia panda kukabiliana na maovu hayo lakini cha muhimu, akasema, ni vijana kupewa mwongozo wa maisha.
“Ama kwa hakika kila mmoja ana jukumu la kuzungumza na vijana hawa ili waweze kujiepusha na ulevi wa kupindukia na utumizi wa dawa za kulevya,” alieleza Bi Rigathi.
Aliyasema hayo katika shule ya M-Pesa Foundation mjini Thika alipofika kuzindua wakfu wa Rose Kirika Foundation.
Alimpongeza Bi Kirika huku akisema mpango wake wa kuwajali walioathirika na pombe na dawa za kulevya ni zawadi kubwa kwa jamii.
“Mimi nimekuwa mstari wa mbele kutetea vijana walioathirika na ulevi na utumizi wa mihadarati,” alisema.
Alisema lengo lao kuu ni kuhakikisha vijana wanaonasuliwa kwa ulevi wanapelekwa masomoni kufanya kozi za kuwawezesha kupata ajira.
Bi Kirika ambaye alijitaja kama Bi Talanta, alisema kilichomchochea kuzindua wakfu wa Rose Kirika Foundation ni kushuhudia walevi wengi wakihudhuria mikutano ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
“Nilijiuliza maswali mengi sana na baadaye nikasema moyoni iwapo Gavana Kimani Wamatangi na mimi tungechaguliwa, ningewasaidia walevi kujiepusha na tabia hiyo,” alifafanua Bi Kirika.
Alisema familia nyingi zinakosana na kusambaratika kwa sababu ya pombe.
Alisema wakfu huo sio wa kupata faida ya kifedha kwa vyovyote vile bali ni wa kusaidia jamii kwa ujumla.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na manaibu wa magavana sita kutoka maeneo tofauti. Nao ni Reuben Kamuri wa Laikipia ambaye ni mwenyekiti wa manaibu gavana kote nchini, Njoroge Muchiri wa Nairobi, na Christine Kilalo wa Taita Taveta.
Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni wachungaji wa makanisa wakiongozwa na maaskofu kadhaa na wadau katika sekta ya biashara hapa nchini.