• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
DPP awasilisha ombi Mkenya apelekwe Marekani kushtakiwa kwa mauaji

DPP awasilisha ombi Mkenya apelekwe Marekani kushtakiwa kwa mauaji

NA RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga amewasilisha rasmi ombi la kumpeleka nchini Marekani mwanamume Mkenya anayesakwa kushtakiwa kwa mauaji ya mpenziwe.

Mwanamume huyo anadaiwa kutekeleza uhalifu huo mnamo Oktoba 31, 2023, kabla ya kutorokea humu nchini.

Bw Ingonga aliwasilisha ombi hilo mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani, Nairobi Bw Lucas Onyina.

Kupitia kwa wakili wa serikali Vincent Monda, DPP alimweleza Bw Onyina kwamba Wizara ya Mashauri ya Kigeni na Ushirikiano wa Kimataifa ilipokea ombi kutoka kwa ubalozi wa Marekani kwamba Bw Kevin Adam Kinyanjui Kang’ethe akamatwe na kurudishwa nchini humo kushtakiwa kwa mauaji ya Margaret Mbitu.

Inadaiwa kwamba Bw Kang’ethe alimchukua Mbitu kutoka mji wa Halifax ulioko maili 60 kutoka mji wa Lowell alipokuwa akiishi mnamo Oktoba 30, 2023.

Marehemu alikuwa akitoa huduma za kiafya Halifax.

Walisafiri ndani ya gari la Bw Kang’ethe muundo wa Toyota Venza lenye rangi nyeupe hadi makazi yake mjini Lowell.

Mbitu aliyekuwa na umri wa miaka 31 alikuwa mpenziwe Bw Kang’ethe.

Inadaiwa Bw Kang’ethe alimuua Mbitu na kumweka kwenye kiti cha mbele cha gari hilo kisha akaliegesha katika garaji la uwanja wa ndege wa kimataifa wa Boston Logan.

Mshukiwa huyu alifunga gari hilo na kumwacha marehemu ndani ya gari hilo kisha akatorokea Kenya.

Akiwasilisha ombi Bw Kang’ethe arudishwe Marekani atakaposhtakiwa Bw Monda alimweleza hakimu, ofisi ya DPP ilipokea ombi rasmi kutoka kwa ubalozi wa Marekani kwamba Mkenya huyo anasakwa kushtakiwa kwa mauaji ya Mbitu.

“Ofisi ya DPP imepokea ombi rasmi kutoka ubalozi wa Marekani, Nairobi kupitia Wizara ya Masuala ya Kigeni, ikiomba Bw Kang’ethe asafirishwe hadi jimbo la Massacheussets kushtakiwa kwa mauaji ya Margaret Mbitu,” Bw Monda alimweleza hakimu mnamo Alhamisi.

Bw Monda alifafanua kwamba mnamo Jumatano, Bw Kang’ethe aliagizwa na hakimu mwandamizi Bi Zainab Abdul azuiliwe kwa siku 30 katika kituo cha polisi cha Muthaiga.

Bw Monda pia aliomba mahakama itoe mwelekeo wa utaratibu utakaofuatwa kuendeleza suala hilo.

Lakini ombi la kumpeleka Bw Kang’ethe nchini Marekani lilipingwa vikali na mawakili watatu wanaomwakilisha.

Mahakama iliombwa imwachilie Bw Kang’ethe kwa dhamana lakini DPP akapinga akisema tayari kuna agizo kwamba mshukiwa huyo azuiliwe kwa siku 30 katika kituo cha polisi cha Muthaiga kabla ya kupelekwa nchini Marekani.

“Napinga mshukiwa huyu akiachiliwa kwa dhamana. Tayari kuna agizo asalie katika korokoro ya polisi hadi Machi 4, 2024, atakaporudishwa kortini kwa maagizo zaidi,” alisema Bw Monda.

Mawakili wanaomwakilisha Bw Kang’ethe waliomba aachiliwe kwa dhamana kabla ya utaratibu wa kumsafirisha hadi Marekani kukamilishwa.

Ombi hilo lilikataliwa mara moja na Bw Onyina akiongeza, “tayari kuna agizo Bw Kang’ethe azuiliwe kwa siku 30.”

Bw Kang’ethe hakupinga ombi azuiliwe kwa siku 30 alipofikishwa mbele ya Bi Abdul mnamo Jumatano.

DPP amewasilisha hati ya kiapo kusema Bw Kang’ethe azuiliwe kwa siku 30 kwa vile akiachiliwa anaweza kutoroka.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Februari 5, 2024, DPP awasilishe tetesi zake kisha mawakili wanaomtetea Bw Kang’ethe wajibu na uamuzi kutolewa endapo Bw Kang’ethe atapelekwa kushtakiwa nchini Marekani au la.

  • Tags

You can share this post!

Jomo, mwanawe Uhuru aondoa kesi aliyoshtaki serikali

Wavinya alaani hatua ya kanjo kukazia madiwani maisha

T L