• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 10:37 AM
DPP awasilisha notisi ya rufaa kupinga Jacque Maribe kuondolewa kosa la mauaji

DPP awasilisha notisi ya rufaa kupinga Jacque Maribe kuondolewa kosa la mauaji

NA RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga amewasilisha notisi ya kukata rufaa kupinga uamuzi wa mahakama kumwachilia aliyekuwa mtangazaji wa runinga ya Citizen Jacque Maribe katika kesi ya mauaji ya kinyama ya mfanyabiashara Monicah Nyawira Kimani.

“Fahamu kwamba Jamhuri, ambayo hapa ni anayenuia kukata rufaa, kwa kutoridhishwa na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Nairobi (Jaji G. Nzioka) uliotolewa jijini Nairobi mnamo Februari 9, 2024, inataka kupinga sehemu ya uamuzi ambapo mshtakiwa wa pili aliondolewa kosa,” imesema notisi ya DPP.

Bi Maribe na Joseph Irungu almaarufu Jowie, walishtakiwa kwamba walitekeleza mauaji ya Monicah mnamo Septemba 19, 2018.

Lakini mnamo Ijumaa, Jaji Grace Nzioka alitoa uamuzi wake ambapo alimpata Jowie na hatia ya kutekeleza mauaji hayo, huku Bi Maribe akiponea.

Jaji Nzioka alianza kueleza kwa muhtasari ushahidi wa kutoka watu 35 waliofika kortini kutegua kitendawili cha mauaji hayo ya kinyama ya Monicah ambaye alikuwa na umri wa miaka 28 alipouawa.

“Nataka tuelewane… sitasoma uamuzi wote neno kwa neno lakini nitasimulia barabara ushahidi ambao nimeuchambua,” alisema Bi Nzioka.

Wote waliofika kortini walishangazwa na jaji huyo aliyeusoma uamuzi huo kwa ustadi na kusimulia sheria kama nyanya anavyowasimulia wajukuu hadithi.

Bi Nzioka hata hivyo alisema washtakiwa wote wawili–Jowie na Bi Maribe–walidanganya katika kuandikisha taarifa na wakati wa kujitetea.

Alisema Bi Maribe alidanganya kwamba Jowie, ambaye wakati huo alikuwa mpenziwe, alikuwa ameshambuliwa na majambazi usiku wa Septemba 20, 2018.

Madai ya Bi Maribe yalikinzana na kauli za walinzi wa mtaa wa Royal Park Estate ulioko Lang’ata.

Mtangazaji huyo aliandikisha taarifa kwa polisi kwamba Jowie alishambuliwa na majambazi lakini akabadili nia na kusema alijipiga risasi begani.

Ni kufuatia kupeana taarifa hiyo ya uongo ndipo Bi Nzioka alimwambia DPP ana wajibu wa kumshtaki Bi Maribe kwa kudanganya polisi ambao kwa kawaida ni maafisa wa umma. Huo ni ukiukaji wa ibara 129 ya kanuni ya adhabu.

“Nimepata kwamba ushahidi dhidi ya mshtakiwa wa pili (Bi Maribe) haitoshi kuthibitisha alitekeleza shtaka dhidi yake na hivyo basi ninamuondolea kosa,” Bi Nzioka akasema.

Jaji huyo alisema Jowie alidanganya pia kwamba alishambuliwa na majambazi. Pia alidanganya kwamba jina lake ni Dominic Bisera Harun.

Jaji huyo alimwachilia Bi Maribe kwa shtaka la kuua na akasema upande wa mashtaka ulikuwa umemfungulia mashtaka yasiyostahili.

Aidha jaji alifuta bondi ya Jowie baada ya uamuzi kubainisha ndiye alitekeleza mauaji na akaagiza azuiliwe katika gereza la Industrial Area, Nairobi kusubiri hukumu mnamo Machi 8, 2024.

Baada ya kusomwa kwa uamuzi, kaka yake Monicah, Bw George Kimani, alisema “haki imetendeka”.

  • Tags

You can share this post!

Sababu za korongo kuondoka Ziwa Nakuru

Mwadime awatetea mawaziri wanaoshinikizwa kujiuzulu kwa...

T L