Habari za Kitaifa

Duale, Maraga wajiunga na viongozi wanaomponda Mudavadi kwa kupendekeza refarenda

Na BENSON MATHEKA December 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI wa Afya, Aden Duale na Jaji Mkuu Mstaafu David Maraga wamejiunga na viongozi wanaokosoa wazo la Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi, la kufanya uchaguzi mkuu wa 2027 pamoja na kura ya maamuzi ya kurekebisha katiba.

Katika mahojiano na runinga ya humu nchini wiki jana, Mudavadi alipendekeza kuwa baadhi ya masuala ya kikatiba ambayo hayajakamilika yanaweza kushirikishwa katika kura ya maamuzi ili wananchi waamue watakapopiga kura katika uchaguzi mkuu ujao.

“Tunaweza kutumia uchaguzi wa 2027 kama mfano wa kwanza kufanya maamuzi kuhusu baadhi ya masuala ambayo hayajakamilika kwenye Katiba ya 2010. Ikiwa tutaweka vizuri maswali hayo kwenye karatasi za kura, wananchi wana akili na uwezo wa kutoa maamuzi sahihi,” Bw Mudavadi alisema.

Aliongeza kuwa masuala kama Ofisi ya Waziri Mkuu, ripoti ya Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (NADCO) na jinsi ya kushughulikia Hazina ya Serikali ya Kitaifa ya Maeneo-bunge (NG-CDF) yanaweza kutatuliwa kupitia kura ya maamuzi.

“Hii itapunguza urasimu wa Bunge na Mahakama, kuongeza ushiriki wa wananchi, na kuokoa rasilimali za serikali,” alisema.

“Kura ya maamuzi inaweza kuwa njia bora ya kujumuisha wananchi katika masuala ambayo yamekuwa mjadala wa muda mrefu.”

Kauli yake ilikosolewa na viongozi kadhaa wa upinzani waliomlaumu kwa kupuuza masuala mazito yanayoumiza Wakenya.

Hata hivyo, ni kauli ya Waziri Duale kumkosoa inayotarajiwa kuzua gumzo.

Jana, Bw Duale alikosoa wazo la Mudavadi akieleza hatari zinazoweza kutokea endapo hatua hiyo itafanywa bila mwongozo wa kisheria.

“Wazo la kufanya kura ya maamuzi bila mwongozo wa Mahakama ya Juu na Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) linaweza kuzua mzozo badala ya kutatua changamoto zilizopo,” alisema Bw Duale.

Kulingana na Bw Duale, si kila suala linafaa kushirikishwa katika kura ya maamuzi.

“Kifungu cha 255 cha Katiba kinasema wazi ni masuala gani yanayopaswa kufanyiwa kura ya maamuzi, na hatua yoyote lazima izingatie viwango hivi vya kikatiba.”

Duale pia alisisitiza kuwa baadhi ya masuala yanayohusiana na utaratibu wa maendeleo na utekelezaji wa kanuni ya thuluthi tatu kuhusu jinsia katika uwakilishi tayari yanashughulikiwa kupitia michakato ya kisheria ya Bunge.

“Kufanyia kura ya maamuzi masuala yanayoshughulikiwa na Bunge kunaweza kudhoofisha michakato hii halali na kuleta usumbufu,” alisema.

Aidha, alibainisha kuwa Kenya bado haina sheria kamili ya jinsi kura ya maamuzi inavyopaswa kufanyika, jambo ambalo linafanya hatua hiyo kuwa hatari na kudhoofisha mfumo wa kisheria.

Jaji Mkuu Mstaafu David Maraga, naye alikosoa Mudavadi, akisisitiza kuwa nchi haiko kwenye mgogoro wa kikatiba, bali inakabiliwa na upungufu wa uongozi, uwajibikaji na utekelezaji.

Katika taarifa aliyotoa jana, Maraga alisema Katiba iko hatarini tena, akilaumu utawala wa sasa kwa kutafuta mabadiliko ya kikatiba kwa maslahi ya kisiasa badala ya maslahi ya wananchi.

Kiongozi huyo wa United Green Movement amesisitiza kuwa msukumo wa marekebisho ni jaribio la kuongeza ushawishi wa kisiasa wa Rais William Ruto.

“Matamshi ya hivi karibuni ya maafisa wa ngazi ya juu wa serikali, akiwemo Bw Musalia Mudavadi, kuhusu haja ya kubadilisha au kurekebisha Katiba yetu ni tamthilia ya kisiasa na dharau isiyo ya kimasomaso kwa Katiba inayoshikilia matumaini yasiyotekelezwa ya wananchi,” Maraga alisema katika taarifa.

Wakati huo huo, kiongozi wa chama cha PLP Martha Karua ameapa kupinga jaribio lolote la aina hiyo.

“Wito wa kura ya maamuzi ni hadaa. Mudavadi, anayetoa wito wa kura ya maamuzi kwa niaba ya Rais Ruto, yeye mwenyewe anashikilia wadhifa usio halali kikatiba,” alisema Bi Karua.

Aliongeza: “Wakenya hawapaswi kukubali mabadiliko ya Katiba kutoka kwa utawala ambao hauitii Katiba.”